Habari

Ujumbe wa Chuo cha Twente Uholanzi Wawasili Tanzania Kuimarisha Ushirikiano wa Kitaalamu

Ujumbe wa Chuo cha Twente Uholanzi Wawasili Tanzania Kuimarisha Ushirikiano wa Kitaalamu
Apr, 17 2026

Ujumbe wa wataalamu kutoka Chuo cha Twente cha nchini Uholanzi umewasili nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika masuala ya upangaji na usimamizi wa ardhi.

Ujumbe huo unatoka katika Kitivo cha Geo-Information Science and Earth Observation (ITC) ukiwa na wataalamu wawili ambao ni Dkt. Johannes Flacke, profesa mshiriki, pamoja na Andre da Silva Mano, mhadhiri, wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya taarifa za kijiografia (GIS) na usimamizi wa ardhi.

Lengo kuu la ziara hiyo ni kujenga uwezo wa kitaalamu kwa watumishi wa Tume, pamoja na kuanzisha na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya tafiti na mafunzo, hususan katika kozi za usimamizi wa ardhi na matumizi ya teknolojia katika upangaji matumizi ya ardhi.

Akizungumza wakati wa kupokea ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph Mafuru, ameeleza maeneo mbalimbali yenye uhitaji wa ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya taarifa za kijiografia, tafiti shirikishi na uendelezaji wa rasilimali watu.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Tume, sambamba na kuimarisha uwezo wa watumishi katika kukabiliana na changamoto za upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.

Kwa upande wao, wajumbe wa Chuo cha Twente wameeleza utayari wao wa kushirikiana na Tume katika maeneo mbalimbali ya kitaaluma, ikiwemo kubadilishana uzoefu, kufanya tafiti za pamoja na kutoa mafunzo yatakayochangia kuboresha sekta ya ardhi nchini.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuimarisha upangaji wa matumizi ya ardhi na usimamizi endelevu wa rasilimali, hatua itakayochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.