Habari
Dkt. Akwilapo afungua rasmi jukwaa la wadau, asisitiza utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya ardhi kwa vitendo
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo (Mb), amefungua rasmi Jukwaa la Wadau wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi 2026, akisisitiza umuhimu wa kuhamisha nguvu kutoka katika hatua ya upangaji wa mipango kwenda kwenye utekelezaji wake kwa vitendo ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mhe. Dkt. Akwilapo alieleza kuwa kauli mbiu ya jukwaa hilo inalenga kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi haiishii kwenye makaratasi bali inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii. Alisisitiza kuwa upangaji bora wa matumizi ya ardhi ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi.
Waziri alibainisha mafanikio yaliyofikiwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), ikiwemo vijiji 4,925 kati ya vijiji 12,333 nchini kuwa tayari vina mipango ya matumizi ya ardhi, pamoja na utoaji wa zaidi ya Hati 40,000 za Hakimiliki za Kimila (CCROs) katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Hata hivyo, alisisitiza haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia vijiji vilivyobaki.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), pamoja na kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuhamasisha wananchi kushiriki katika gharama za upimaji na umilikishaji wa ardhi ili kuongeza ufanisi na umiliki shirikishi.
Katika maelekezo yake, Waziri aliiagiza Tume kuongeza juhudi katika kuwezesha upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi ili kupunguza au kuondoa kabisa migogoro ya matumizi ya ardhi. Pia alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa vikao vya ngazi za kanda kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa mipango hiyo, huku akiagiza Ofisi ya Waziri kupatiwa nakala ya maazimio ya wadau kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu na wenye tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, alieleza kuwa Mkoa huo unakabiliwa na changamoto za kimazingira, hususan katika Bonde la Kilombero, ambako shughuli za kibinadamu zimechangia uharibifu wa mazingira na kusababisha migogoro ya matumizi ya ardhi miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii.
Awali, akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph Mafuru, aliwashukuru wadau wote kwa ushiriki wao na kueleza kuwa Serikali imeendelea kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake, hususan katika maeneo ya vijijini ambako shughuli nyingi za kiuchumi hufanyika
Alisisitiza umuhimu wa upangaji wa matumizi ya ardhi ulio jumuishi na shirikishi, huku akibainisha kuwa bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu, ufinyu wa rasilimali fedha na matumizi hafifu ya teknolojia. Aliongeza kuwa jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa wadau kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha sekta ya ardhi.
Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali wakiwemo TISEZA, AWF, IUCN na CRDB walitoa salamu zao, wakipongeza juhudi za Tume na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano ili kuharakisha uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa lengo la kufikia Dira ya Taifa 2050.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano wa wadau, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, kupunguza migogoro, na hatimaye kuchangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini.
