Habari

NLUPC na FORLAND Wasaini Makubaliano ya Ushirikiano kuwezesha Uandaaji wa VLUPs katika Vijiji vya CBFM

NLUPC na FORLAND Wasaini Makubaliano ya Ushirikiano kuwezesha Uandaaji wa VLUPs katika Vijiji vya CBFM
Feb, 14 2026

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) na Forestry, Land Use and Value Chains Development in Tanzania (FORLAND) wamesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa lengo la kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji (VLUPs), hususan katika Vijiji vinavyotekeleza Usimamizi wa Misitu kwa Jamii (Community Based Forest Management – CBFM).

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika tarehe 13 Februari 2025 katika Jiji la Iringa, ikihudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka pande zote mbili. Ushirikiano huu unalenga kuongeza ufanisi katika upangaji na usimamizi bora wa matumizi ya ardhi kwa kuzingatia uhifadhi wa rasilimali za asili, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu ya Vijiji.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC, Bw. Joseph C. Mafuru, amesema kuwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuendeleza jitihada za Serikali za kuhakikisha ardhi inapangwa na kutumika kwa njia shirikishi, inayozingatia mahitaji ya wananchi na uhifadhi wa mazingira.

“Makubaliano haya yataisaidia Serikali katika jitihada zake za kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi inayozingatia uhifadhi wa misitu, vyanzo vya maji, maeneo ya malisho na rasilimali nyingine muhimu, sambamba na kuwezesha matumizi endelevu ya ardhi kwa shughuli za kijamii na kiuchumi,” amesema Bw. Mafuru.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa FORLAND, Bw. Andrew Ferdinands, amesema kuwa programu hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na NLUPC katika kutoa msaada wa kitaalamu kwa Mamlaka za Upangaji pamoja na kubadilishana uzoefu, ili kuhakikisha Mipango ya Matumizi ya Ardhi inaandaliwa kwa viwango bora na vinavyokubalika Kitaifa.

Bw. Ferdinands ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, pande zote mbili zitafanya kazi kwa karibu katika kusimamia na kutoa mwongozo wa kitaalamu kwa Timu za Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi za Wilaya wakati wa utekelezaji wa hatua mbalimbali za uandaaji wa VLUPs, kwa kuhakikisha matumizi yote ya ardhi yanazingatiwa ipasavyo, ikiwemo hifadhi za misitu ya Vijiji, maeneo ya uhifadhi wa mazingira na bioanuwai.

FORLAND ni mpango wa miaka minne unaofadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Finland, ukitekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT). Mradi huo unalenga kukuza sekta ya misitu endelevu na shirikishi inayochangia ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, mradi wa FORLAND unatarajiwa kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji takribani 160, katika Halmashauri za Wilaya 20 zilizopo kwenye Mikoa minne ya Ruvuma, Iringa, Njombe na Lindi.

Utekelezaji wa makubaliano haya unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu na ardhi, kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za misitu kwa jamii na wajasiriamali wadogo, pamoja na kuunga mkono juhudi za Taifa katika kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.