Habari
NLUPC, IUCN Wajadili Ushirikiano Utekelezaji Mradi wa Suluhisho Asilia (NBS)
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) na Shirika la Uhifadhi la International Union for Conservation of Nature (IUCN) wamefanya kikao kwa ajili ya kuanzisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ardhi, kilichofanyika Jumatano, Aprili 16, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Tume Jijini Dodoma.
Kikao hicho kililenga kujadili utekelezaji wa mradi wa Resolve NbS (Nature-Based Solutions) pamoja na kubaini fursa mpya za ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili katika masuala ya mipango ya matumizi ya ardhi na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Mwakilishi wa IUCN nchini Tanzania, Anthony Mhagama, alisema kuwa mradi wa Resolve NbS unahusiana moja kwa moja na mipango ya matumizi ya ardhi, ukiwa na muda wa utekelezaji wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2025 hadi 2027, na unafadhiliwa na Norwegian Agency for Development Cooperation.
Kwa upande wake, Afisa Programu wa IUCN, Sharon Kishenyi, alieleza kuwa mradi huo utatekelezwa katika mikoa ya Morogoro na Iringa, ukilenga kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula pamoja na uhifadhi wa mifumo ya ikolojia. Aidha, alisema mradi huo utasaidia kupunguza athari za majanga ya mazingira yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa mradi wa Resolve NbS unalenga kuongeza uelewa kwa jamii na wadau kuhusu upangaji na utekelezaji wa suluhisho asilia, huku ukihakikisha dhana hiyo inaingizwa kikamilifu katika sera na utekelezaji wake. Pia, mradi huo unakusudia kupunguza changamoto za upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa suluhisho hizo.
Naye Afisa Programu wa IUCN, Abdulaziz Mkwizu, alisema kuwa mradi huo unahusisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo uandaaji na uhuishaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika ngazi ya vijiji, pamoja na kuimarisha usimamizi wa mipango iliyopo.
Alibainisha kuwa mradi huo pia unaipa kipaumbele utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) kwa wanawake, akisisitiza umuhimu wake katika kukuza usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kilijadili rasimu ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya Tume na IUCN, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.
Akiwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi Mkuu baada ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu (DLUPMC), Bw. Jonas Masingija Nestory, alisema kuwa ushirikiano huo utajikita katika maeneo muhimu ikiwemo uandaaji wa mikutano ya wadau, uimarishaji wa uwezo wa wataalamu kuanzia ngazi ya kitaifa hadi jamii, uandaaji wa mipango bora ya matumizi ya ardhi, utatuzi wa migogoro ya ardhi, pamoja na uhamasishaji wa rasilimali.
Aliongeza kuwa maeneo mengine yatakayozingatiwa ni pamoja na uandaaji wa mipango kina, utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs), pamoja na kufanya tafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango hiyo.
Hatua inayofuata ni kusaini makubaliano rasmi ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili, zoezi linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni, likilenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo endelevu ya ardhi nchini.
