Habari

Watumishi NLUPC Waungana na Wafanyakazi nchini kuadhimisha Meimosi

Watumishi NLUPC Waungana na Wafanyakazi nchini kuadhimisha Meimosi
May, 12 2026

Watumishi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) leo Mei 01, 2026, wameungana na wafanyakazi wengine nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Meimosi), wakisisitiza umuhimu wa bidii, mshikamano na uzalendo katika kulijenga Taifa.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri, yakianza na maandamano kutoka eneo la Bunge kuelekea uwanjani, jijini Dodoma, ambapo makundi mbalimbali ya wafanyakazi kutoka sekta za umma na binafsi yalijitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ambaye katika hotuba yake aliwataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uzalendo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya kazi, ubunifu na uwajibikaji ili kuchochea maendeleo ya Taifa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, alihimiza waajiri kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha haki na ustawi wa wafanyakazi unazingatiwa, jambo litakalosaidia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Watumishi wa Tume walionesha mshikamano na ari ya kazi kwa kushiriki kikamilifu katika maandamano na shughuli mbalimbali za siku hiyo, wakibeba mabango yenye ujumbe unaohamasisha utendaji kazi wenye weledi na upangaji matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu.

Ushiriki wao umeakisi dhamira ya taasisi hiyo katika kuendelea kusimamia na kuratibu upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Maadhimisho ya Meimosi yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya Taifa, pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya wafanyakazi na waajiri kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kazi, yenye usawa, heshima na tija.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba Kauli Mbiu:

“Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”

Kauli mbiu hiyo inaakisi umuhimu wa kuhakikisha wafanyakazi wanapata mazingira bora ya kazi, haki zao zinazingatiwa, na mchango wao unatambuliwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya Taifa.