Habari

Baraza la Wafanyakazi lajadili utendaji na kuweka Mikakati ya Kuboresha Huduma za Tume

Baraza la Wafanyakazi lajadili utendaji na kuweka Mikakati ya Kuboresha Huduma za Tume
May, 12 2026

Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), leo Mei 07, 2025, limekutana kujadili utekelezaji wa majukumu ya Tume na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi katika kipindi kijacho.

Katika kikao hicho, wajumbe wa Baraza walipata fursa ya kujadili mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Tume, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa shughuli za upangaji wa matumizi ya ardhi pamoja na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa baadhi ya shughuli.

Wajumbe walisisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubunifu katika utendaji wa kila siku ili kufikia malengo ya taasisi.

Aidha, wajumbe walijadili na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma zinazotolewa na Tume, ikiwemo kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa, kuboresha mifumo ya kazi, na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Vilevile, Baraza la Wafanyakazi limeazimia kuimarisha ushirikiano kati ya watumishi na uongozi wa Tume, pamoja na kubuni mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuongeza ufanisi wa taasisi na kuboresha maslahi ya watumishi.

Baraza pia lilisisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga uwezo wa watumishi kupitia mafunzo endelevu, ili kuongeza weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya pamoja ya kuhakikisha Tume inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji, sambamba na kuimarisha huduma za upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi nchini.