Habari
Hatimiliki 6000 Kutolewa kwa Wananchi wa Vijiji 10

Wananchi zaidi ya 6000 waliopo katika Vijiji 10 vilivyopo kwenye Halmashauri za Wilaya 10 nchini wanatarajiwa kumilikishwa ardhi zao Kisheria kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) hali itakayosaidia wananchi hao kuwa na Milki salama za maeneo yao, kuepuka migogoro ya matumizi ya ardhi pamoja na kutumika Hatimiliki hizo kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika Kikao Kazi baina yake na wataalamu wa Tume wanaokwenda kuwezesha zoezi hilo kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya husika, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume CPA. Esther Subbi amewataka wataalamu hao kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kuwezesha kukamilisha zoezi hilo kwa wakati na wananchi waweze kumilikishwa vipande vya ardhi zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Uratibu na Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi Bw. Dioscory Kanuti amesema kuwa umilikishaji wa ardhi za wananchi hao ni njia mojawapo ya kuwahakikishia umiliki salama wa maeneo yao, kuepusha migogoro pamoja na kuwawezesha wananchi hao kuwa na ujasiri wa kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi.
Halmashauri za Wilaya zitakazonufaika katika zoezi hilo ni Ruangwa (Lindi), Ikungi (Singida), Kishapu (Shinyanga), Korogwe (Tanga) na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe iliyopo Mkoani Katavi.Kupitia zoezi hilo, kila Halmashauri ya Wilaya itajumuisha vijiji 2 ambapo katika kila Kijiji, wananchi 600 watapatiwa Hatimiliki.