Habari
Tume yaanza Ukaguzi wa Uzingatiaji Upangaji Matumizi ya Ardhi katika Vijiji 20
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeanza kazi ya Ukaguzi wa Uzingatiaji (Compliance Auditing) wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiji 20 vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya tatu za Mkoa wa Dodoma.
Zoezi hilo linatarajiwa kubaini kiwango ambacho Mipango hiyo imezingatia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo, Taratibu na Vigezo vilivyowekwa katika Uandaaji, Utekelezaji na Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, hali itakayowezesha Tume kutoa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kuboresha Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika ngazi ya Vijiji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu katika kikao kazi cha maandalizi ya zoezi hilo, Mkurugenzi wa Utafiti, Uzingatiaji na Mifumo ya Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dkt. Joseph Paul, amewataka Wataalamu watakaoshiriki katika kazi hiyo kufanya Ukaguzi kwa kuzingatia weledi, na maadili ya taaluma.
Dkt. Paul amesisitiza kuwa Ukaguzi huo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha kuwa Mipango iliyopangwa inatekelezeka, inalinda maslahi ya wananchi, na inatoa mwongozo sahihi katika matumizi endelevu ya ardhi katika Vijiji.
Alkadharika, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa kazi hiyo ni muhimu kwa Taasisi, kwani matokeo ya Ukaguzi huo yatatumika kuboresha mifumo ya Uratibu wa Upangaji, Utekelezaji na Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya ardhi nchini pamoja na kuongeza kasi ya Uandaaji wa Mipango hiyo.
Aidha, amewahimiza Wataalamu hao kutoa tathmini iliyo wazi na yenye ushahidi ili kusaidia Tume kuimarisha ubora wa Mipango husika na kuwezesha Halmashauri kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Halmashauri za Wilaya zitakazohusika na zoezi hilo ni pamoja na ni Bahi, Chemba na Mpwapwa.
Zoezi hilo la Ukaguzi linafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) (0) cha Sheria ya Mipango wa Matumizi ya Ardhi Sura 116 na ni sehemu ya mpango wa Tume wa kuimarisha Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini, sambamba na kuhakikisha kuwa ardhi inatumika kwa tija na kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya kizazi kijacho.
