Habari
Wananchi Manyoni waipa Uhifadhi kipaumbele katika Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imekamilisha zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 16 huku zoezi hilo likiacha alama ya utatuzi wa Migogoro ya mipaka ya vijiji, Wananchi katika Vijiji hivyo wakifanikiwa kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali zikiwemo Hekta 27,826.74 za Uhifadhi wa Misitu na Vyanzo vya Maji, hali itakayosaidia utunzaji wa vyanzo hivyo vinavyotegemewa katika uzalishaji wa umeme nchini.
Imeelezwa kuwa, zoezi hilo limekuja wakati muafaka katika Wilaya hiyo iliyoajaliwa kuwa na rasilimali ardhi muhimu, zikiwemo Mapori ya Akiba ya Wanyamapori, Mimea hadimu pamoja na maeneo makubwa ya Misitu inayowasaidia wanavijiji kufanya biashara ya Hewa Ukaa.
Kiongozi wa zoezi hilo kutoka Tume Bi Suzana Mapunda anabainisha kuwa, kazi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa lengo la Serikali linafanikiwa kupitia ushirikishwaji wa wananchi katika kuamua ardhi yao itumikaje bila kuathiri Mazingira pamoja na Uhifadhi
Kwa upande wao, wananchi wa Vijiji hivyo wameshukuru kwa ujio wa zoezi hilo kwani utawasaidia kutambua maeneo yao ya kufanyia shughuli mbalimbali ili kuondokana na migogoro ya ardhi na litawasaidia kumiliki ardhi kisheria.
Kukamilika kwa zoezi hilo Wilayani Manyoni lililowezeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi linafungua ukurasa mwingine wa utekelezaji wa kazi kama hiyo kwenye Vijiji vingine 16 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.