Habari

Hekari 200,000 Zapatikana kwa Ajili ya Malisho Katika Wilaya ya Kiteto Kupitia Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Hekari 200,000 Zapatikana kwa Ajili ya Malisho Katika Wilaya ya Kiteto Kupitia Mipango ya Matumizi ya Ardhi
Nov, 18 2018

Hekari zaidi ya laki mbili kwa ajili ya malisho ya mifugo zimetengwa kupitia mpango wa pamoja ya matumizi ya ardhi ya vijiji (joint village land use plans) vya Amei, Loolera, Lembapuli na Lesoit Wilayani Kiteto utakaojulikana kama ALOLLE.

Ukanda huu wa malisho uliopatikana kupitia mradi wa SRMP (Sustainable Rangeland Management Project) ni hatua muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya malisho itakayowezesha kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi inayotokea mara mara baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dkt. Stephen Nindi amesema kuwa Serikali imeweka mkazo katika upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuepuka muingiliano wa shughuli za ardhi na kuifanya ardhi kuwa ya uzalishaji ili kuchangia kwenye maendeleo ya kiuchumi pamoja na uhifadhi wa mazingira.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji inafanyika ili kuboresha uzalishaji, kutunza mazingira ya bionuai na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi nchini. Kutengwa kwa ardhi ya malisho kwa ajili ya jamii za wafugaji kutapunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kama vile wakulima, mamlaka za hifadhi na wawekezaji pamoja na kusaidia maendeleo ya kiuchumi na usimamizi endelevu wa nyanda za malisho.” Alisisitiza Dkt. Nindi

Jitihada hizi ni muendelezo wa kufanikisha malengo ya Serikali pamoja na wadau wake katika kuhakikisha upangaji wa matumizi ya ardhi kwenye kila kipande cha ardhi ili kuondoa muingiliano wa shughuli kuu zitumiazo ardhi. Hapo awali, mpango kama huu ulifanikisha kupatikana kwa hekari 75,000 katika vijiji vya Orkitikiti, Lerug, Ngapapa na Engang’uengare vilivyopo Wilayani Kiteto ukanda wa malisho ujulikanao kama OLENGAPA.