Habari
Awamu ya Sita yavunja rekodi Upangaji Matumizi ya Ardhi ya Vijiji

SERIKALI kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imevunja rekodi ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 2,480 kwa kipindi cha muda mfupi wa miaka minne kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 ikilinganishwa na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 1,269 iliyoandaliwa miaka ya nyuma toka kuanzishwa kwa Tume.
Hayo yamebainishwa Juni 23, 2025 Jijini Arusha na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi, Anthony Sanga kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ufunguzi wa jukwaa la wadau mbalimbali wanaojihusisha na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kutoka Serikalini na sekta binafsi.
Mhandisi Sanga alisema kuwa Wizara yake haina budi kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea fedha Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ambapo hadi sasa imewezesha kuandaa Mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 4,679 kati ya vijiji 12,333 hali inayopelekea kusalia kwa Vijiji 7,654 ambavyo havijaandaliwa Mipango hiyo.
Aidha, ili kufanikisha kumaliza uandaaji wa Mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji vyote nchini, Mhandisi Sanga alitoa wito kwa Wadau kuendelea kuunganisha nguvu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuandaa Mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na Serikali. Vilevile, Katibu Mkuu huyo aliziasa Halmashauri za Wilaya nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuandaa Mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji vyao.
"Hili ni jambo kubwa la kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa utoaji wa fedha kwa Tume na kuwezesha Vijiji hivyo kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi na kuwashukuru wadau kutoka sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali katika kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro ya ardhi baina ya makundi mbalimbali"
Ametilia mkazo kuwa wizara ya ardhi itaendelea kuhuisha ramani za msingi zilizokuwepo tangu miaka ya 70 zilizopo nchi nzima ili kuwa na ramani bora sanjari na ununuzi wa ndege na droni ikiwemo utoaji wa hati za Kimila na kuboresha vituo vya upimaji vya kieletroniki ili kurahisisha upangaji na upimaji wa miji na vijiji ikiwemo maeneo mengine muhimu kwa ustawi wa jamii
Akisoma taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Joseph Mafuru, Mkurugenzi wa Utafiti na Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dkt. Joseph Paul alisisitiza wadau hao kushirikiana na Tume kwa ajili ya kupanga maeneo ya Vijiji na miji ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana ikiwemo kutenga maeneo ya ya matumizi mbalimbali ikiwemo malisho, kilimo, huduma za Kijamii na mengieyo.