Habari
Nyangh’wale yatambua Mchango wa Tume katika Upangaji Matumizi ya Ardhi
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Grace Kingalame, umeitunuku Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) tuzo ya shukrani kwa kutambua jitihada zake katika kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji pamoja na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi tuzo hiyo, Mhe. Kingalame, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Nyang’hwale yenye jumla ya Vijiji 62, hakuwahi kufanyika zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji wala utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila.
Hata hivyo, katika kipindi cha miezi 24 iliyopita, jumla ya Vijiji 23 vimewezeshwa kuandaliwa mipango hiyo, hali iliyopelekea wananchi 838 kuhakikiwa maslahi ya vipande vyao vya ardhi na kumilikishwa ardhi kisheria kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila hatua iliyochangia kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.
Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Joseph C. Mafuru, Mkurugenzi anayeshughulikia Upangaji Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu, Bw. Jonas Masingija Nestory, alisema kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuendeleza ushirikiano kati ya Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, kwa lengo la kuhakikisha Vijiji vingi zaidi vinawezeshwa kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
Aidha, Bw. Masingija aliweka bayana kuwa Tume imekuwa ikishirikiana na Halmashauri za Wilaya mbalimbali nchini katika kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi, hususan waishio Vijijini, kuondokana na migogoro ya ardhi, kuongeza tija katika shughuli zao za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi kupitia umiliki wa ardhi unaotambulika kisheria.
Tuzo hiyo imetolewa wakati wa hafla ya ugawaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila 838 kwa wananchi wa Vijiji vya Bujula Mienze na Ihushi, Wilayani Nyang’hwale. Zoezi hilo lilitekelezwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
