Habari

Wataalamu NLUPC Wanolewa Matumizi ya Mfumo aa e-Ardhi

Wataalamu NLUPC Wanolewa Matumizi ya Mfumo aa e-Ardhi
Jul, 10 2026

Wataalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi leo, Julai 8, 2026, wameanza kutoa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi kwa wataalamu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa zoezi la kuwezesha uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) kupitia mfumo huo wa kidijitali.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Bw. Joseph C. Mafuru, amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali ni hatua muhimu katika kuimarisha ufanisi, uwazi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi, hususan katika sekta ya ardhi.

Bw. Mafuru amewataka wataalamu wa Tume kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kuongeza ujuzi na uwezo wa kutumia Mfumo wa ILMIS/e-ARDHI kwa weledi, ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Tume na kuhakikisha huduma za umilikishaji wa ardhi zinatolewa kwa haraka, kwa usahihi na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu (DLUPMC), Bw. Jonas Masingija, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kufuatia maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yanayotaka hatimiliki zote za ardhi kuandaliwa kupitia Mfumo wa e-Ardhi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha utoaji wa huduma kwa njia za kidijitali.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Tume inatarajia kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa vijiji 1,492 na kuandaa Mipango Kina 181, ambayo itawezesha utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) 108,600 kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Bw. Masingija amewahimiza wataalamu kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo kwa kujifunza kwa umakini na kutoa maoni ya kitaalamu yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa e-Ardhi, hususan kwa kuzingatia uzoefu walioupata katika matumizi ya Mfumo wa Taifa wa Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUIS).

Amesema maboresho hayo yatachangia kuongeza ufanisi wa mfumo na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi nchini.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuiwezesha Tume kutumia kikamilifu Mfumo wa e-Ardhi katika uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila, hatua inayotarajiwa kuharakisha utoaji wa huduma, kuimarisha usalama wa milki za ardhi na kusaidia utekelezaji wa mipango ya Serikali ya matumizi bora na endelevu ya ardhi nchini.