Habari
AfDB Yaipongeza Tume kwa Mafanikio ya Utekelezaji wa Mradi wa ZORED-VLUP
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipongeza Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mradi wa Zonal, Regional, District and Village Land Use Planning (ZORED-VLUP), unaotarajiwa kukamilika rasmi mwishoni mwa Septemba 2026.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Bi. Maria Saguti-Marealle, wakati wa kikao kazi na Uongozi wa Tume kilichofanyika leo Julai 14, 2026 Jijini Dodoma, kwa lengo la kupokea taarifa ya maendeleo ya mwisho ya utekelezaji wa mradi pamoja na kujadili hatua za kuukamilisha na kuhakikisha matokeo yake yanaendelea kuwa na manufaa kwa Taifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Saguti-Marealle alisema Mkurugenzi wa Idara inayohusika na Usimamizi wa Rasilimali Ardhi wa Benki hiyo ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi na, kwa niaba ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ameipongeza Tume kwa usimamizi mzuri na utekelezaji wenye matokeo chanya.
“Tumepokea taarifa za maendeleo ya mradi na tunapongeza kazi kubwa iliyofanywa na Tume pamoja na wadau wote walioshiriki katika utekelezaji wake. Mafanikio haya yanaweka msingi imara ya upangaji wa matumizi ya ardhi na usimamizi wa rasilimali nchini," alisema Bi. Saguti-Marealle.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Bw. Joseph C. Mafuru, alisema mradi huo umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya upangaji wa matumizi ya ardhi kwa kupanua wigo wa upangaji kutoka ngazi ya Vijiji na Wilaya hadi kufikia ngazi za Kanda na Mikoa.
Alieleza kuwa hatua hiyo imeongeza uwezo wa mamlaka za upangaji nchini katika kuratibu matumizi bora ya ardhi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali za ardhi na kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji, maendeleo ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na matumizi endelevu ya ardhi.
Mradi wa ZORED-VLUP, ambao umetekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024, umefanikiwa kuandaa Mpango mmoja wa Matumizi ya Ardhi wa Kanda, Mipango mitatu ya Matumizi ya Ardhi ya Mikoa, Mpango mmoja wa Matumizi ya Ardhi wa Wilaya, Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 90, pamoja na kuandaa zaidi ya Hati 400 za Hakimiliki za Kimila (CCROs), hatua iliyochangia kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi kwa wananchi na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya mradi.
Mradi huo umefadhiliwa na Korea-Africa Economic Cooperation (KOAFEC) kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kutekelezwa na Tume katika maeneo ya Makete (Njombe), Sumbawanga (Rukwa), Butiama na Musoma (Mara), pamoja na Shinyanga.
Ziara ya ujumbe wa AfDB ni sehemu ya ukaguzi wa mwisho wa maendeleo ya mradi kabla ya kufungwa rasmi, huku pia ikilenga kujadili mikakati ya kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelezwa na kupanuliwa kupitia programu mpya ya DigiLUP-Tanzania, inayotarajiwa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi nchini.
