Habari

NLUPC, ARU Waanza majadiliano ya Mafunzo Maalum ya GIS kwa Wataalamu wa Tume

NLUPC, ARU Waanza majadiliano ya Mafunzo Maalum ya GIS kwa Wataalamu wa Tume
Jul, 03 2026

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) wamekutana kujadili maandalizi ya mafunzo maalum ya matumizi ya Geographical Information System (GIS) yatakayolenga kuwajengea uwezo Wataalamu wa Tume ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Upangaji na Usimamizi wa matumizi ya ardhi nchini.

Kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, CPA. Esther Subbi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph C. Mafuru, huku ujumbe wa Chuo Kikuu cha Ardhi ukiongozwa na Prof. Ally Namangaya, Mkuu wa Shule ya Spatial Planning and Social Sciences (ARU).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, CPA. Subbi aliishukuru ARU kwa kukubali kushirikiana na Tume katika kubuni programu ya mafunzo maalum (Tailor-Made Training), akieleza kuwa ushirikiano huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uwezo wa watumishi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Alisema kuwa utekelezaji wa majukumu ya Tume unahitaji matumizi makubwa ya teknolojia za kisasa za mifumo ya taarifa za kijiografia, ambayo imekuwa nyenzo muhimu katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za maeneo, ufuatiliaji wa matumizi ya ardhi na kufanya maamuzi yanayotegemea takwimu sahihi.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa Tume ina wataalamu kutoka taaluma mbalimbali, zikiwemo mipango ya matumizi ya ardhi, upimaji ardhi na ramani, mazingira, misitu, kilimo, uchumi, sheria, TEHAMA na wengine, hivyo mafunzo hayo yanatarajiwa kuzingatia mahitaji ya kila taaluma ili kuhakikisha kila Mtaalamu anapata ujuzi wa matumizi ya GIS kulingana na majukumu yake ya kazi.

Aidha, alisema Tume inatarajia kupitia majadiliano hayo kufikia muafaka kuhusu muundo wa mafunzo, maudhui yatakayofundishwa, muda wa utekelezaji, mbinu za ufundishaji zitakazojumuisha nadharia na mafunzo kwa vitendo, pamoja na mfumo wa kutathmini matokeo ya programu hiyo.

Kwa upande wake, Prof. Ally Namangaya alieleza utayari wa Chuo Kikuu cha Ardhi kushirikiana na Tume katika kuandaa programu ya mafunzo yenye ubora wa hali ya juu, akibainisha kuwa uzoefu wa chuo katika taaluma za ardhi na teknolojia za taarifa za kijiografia utawezesha kuandaliwa kwa mafunzo yanayokidhi mahitaji halisi ya Tume na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa sehemu ya mkakati wa Tume wa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini, sambamba na kuongeza uwezo wa kitaalamu wa watumishi ili kutoa huduma zenye ufanisi zaidi kwa wananchi na wadau wa sekta ya ardhi.