Habari
Hati za Hakimiliki za Kimila Suluhisho la Migogoro ya Ardhi kwa Wananchi wa Ukerewe
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imewezesha kutolewa kwa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) zaidi ya 1,300 kwa wakazi wa Vijiji vya Namagondo na Busiri vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, hatua inayotarajiwa kuwa suluhisho la migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu katika maeneo hayo.
Hati hizo zimetolewa leo Jumatatu, tarehe 16 Februari 2026, kwa wakazi zaidi ya 700 wa Kijiji cha Namagondo na wengine zaidi ya 500 wa Kijiji cha Busiri, katika hafla iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya (MB), iliyofanyika katika Kijiji cha Namagondo, Wilayani Ukerewe.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa Hatimiliki hizo, Mhe. Mmuya amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha Vijiji vyote nchini vinaandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ili kutokomeza tatizo sugu la migogoro ya ardhi.
Ameeleza kuwa migogoro ya ardhi haina tija kwa maendeleo ya jamii, na amewataka wananchi kuacha kuishabikia migogoro hiyo, badala yake kushirikiana na Mamlaka husika katika kutafuta suluhu za kudumu. Amesisitiza kuwa upangaji shirikishi wa matumizi ya ardhi ni nyenzo muhimu ya kuzuia migogoro, kulinda rasilimali na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kupatikana kwa Hatimiliki hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza na hatimaye kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi iliyokuwa ikisababisha uvunjifu wa amani ndani ya jamii, hali iliyokuwa ikikwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Aidha, wananchi hao wamebainisha kuwa hatimiliki hizo zitawawezesha kutumia ardhi yao kama dhamana katika taasisi za kifedha, hivyo kupata mikopo itakayosaidia kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph C. Mafuru, amesema kuwa kati ya vijiji 16 vilivyoandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika wilaya hiyo, vijiji viwili vya Namagondo na Busiri ndivyo vilivyofanikiwa kuandaliwa mipango ya kina, hatua iliyochangia upatikanaji wa hatimiliki kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Bw. Mafuru ameongeza kuwa miongoni mwa wanufaika wa hatimiliki hizo ni wanawake, vijana, wazee, wajane, wagane na watu wenye ulemavu, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha usawa na ujumuishaji katika umiliki na matumizi ya ardhi.
Kwa mujibu wa takwimu, Mkoa wa Mwanza una jumla ya vijiji 545, ambapo hadi sasa vijiji 160, sawa na asilimia 29.39, vimeandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Halmashauri za Wilaya za Misungwi, Magu, Kwimba, Buchosa na Ukerewe.
Utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi, kupunguza migogoro na kuchochea maendeleo endelevu ya wananchi Vijijini.
