Habari

Kamati ya Bunge Yapongeza Utekelezaji Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi

Kamati ya Bunge Yapongeza Utekelezaji Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi
Mar, 19 2022

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza kazi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vinavyopitiwa na Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) na kuishauri Serikali kuongeza kasi ili mipango hiyo iandaliwe kwenye Halmashauri zote nchini. Kamati hiyo imetoa pongezi hizo Wilayani Singida ikiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi nchini unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).

Ikiwa Mkoani Singida, Kamati hiyo ilitembelea kijiji cha Nkwae ambapo ilipata mawasilisho ya kazi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vya Nkwae na Ntondo kupitia ramani zinazoenyesha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile Makazi, Kilimo, Misitu na mengineyo. Kazi hizo ziliwasilishwa Wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji (VLUMCs) ambao ndio wana jukumu la kusimamia mipango hivyo kwa niaba ya vijiji vyao.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mh. Dkt. Angeline Mabula aliipongeza Kamati ya Bunge kwa maoni na ushauri wanaoutoa mara kwa mara na kueleza kuwa ushauri na maoni yao yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi katika utekelezaji majukumu ya Wizara.

Aidha, Mh. Waziri aliitaarifu Kamati kuwa katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi uliidhinishiwa jumla ya shilingi Bilioni 1.5 ambapo hadi kufikia Februari 2022 jumla ya shilingi milioni 844.5 zilikuwa zimepokelewa. Hadi sasa, utekelezaji mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi umewezesha vijiji 239 vilivyopitiwa na miradi ya kimkakati kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Akijibu baadhi ya hoja za waheshimiwa Wabunge kuhusu kasi ya upangaji matumizi ya ardhi pamoja na taarifa za mipango hiyo katika Halmashauri mbalimbali nchini, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Prof. Wakuru Magigi ameieleza Kamati kuwa Mamlaka za Upangaji kote nchini, zimeelekezwa kutenga bajeti ili kuviwezesha vijiji vyao kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi. Aidha, Prof. Magigi aliiambia Kamati kuwa, kwa sasa Tume inatengeneza Mfumo wa Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini (NLUIS) ambapo kukamilika kwakwe kutasaidia kuweka pamoja taarifa zote za mipango ya matumizi ya ardhi kuanzia ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya hadi Kijiji.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mh. Ally Makoa, amesema Kamati yake imeridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa katika vijiji vya Ntondo na Nkwae na gharama iliyotumika imeleta tija. “Kamati imefika hapa na tumejiridhisha na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali, milioni 28 zilizotumika kwenye vijiji vya Ntondo na Nkwae zimeonyesha tija kubwa mno, kwa maneno waliyoayasema wana Ntondo na Nkwae wenyewe” alisema Mh. Makoa.

Kamati hiyo ilihitimisha ziara yake na zoezi la ugawaji wa Hatimiliki za Kimila (CCROs) kwa wananchi wa vijiji vya Ntondo na Nkwae. Hatimiliki hizo zimeandaliwa katika eneo la Makazi ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, ambapo zaidi ya viwanja 200 vimepimwa na kuandaliwa Hatimiliki.

Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi (Land Use Planning Project) unawezeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia fedha za ndani za Miradi ya Maendeleo. Aidha, katika bajeti ya 2022/2023 utekelezaji wa mradi huo utaendelea kijikita katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vinavyopitiwa na miradi ya kimkakati ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na vijiji vyenye vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji kwenye Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP).