Habari

Makete wahitimisha safari ya Upangaji Matumizi ya Ardhi ya Vijiji

Makete wahitimisha safari ya Upangaji Matumizi ya Ardhi ya Vijiji
Jul, 03 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imekamilisha uwezeshaji wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji arobaini na nne (44) katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete hatua inayotoa fursa kuanza kwa mchakato mwingine wa kuwapimia wananchi mashamba na kuwamilikisha kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila.

Akizungumza katika Mkutano wa Kijiji cha Mpangala, Kata ya Matamba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Bw. William Makufwe ameishukuru Serikali kupitia Tume kwa kuwezesha uandaaji wa mipango hiyo.

“Fursa hii tumepata kupitia Serikali ya awamu ya sita chini ya Mh. Rais, katika kutekeleza huu mradi, taarifa kutoka Tume zinaonyesha kuwa Wilaya ya Makete tumepata vijiji vingi ukilinganisha na Wilaya zingine” alisema Bw. Makufwe

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Halmashauri yake imebahatika kuwa na vijiji vingi vinavyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa wakati mmoja na kuwaasa wananchi kutoa kuchangamkia fursa ya kupimiwa mashamba ili waweze kupata Hatimiliki za kimila.

“Hapo baadae mtapimiwa mashamba yenu na kupatiwa hatimiliki za kimila, hati hizi zitawasaidia kwenye masuala mengi ikiwemo kuondoa migogoro ya ardhi, mtamiliki ardhi kisheria na pia mtazitumia hati hizo kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza mashamba yetu ili muongeze kipato” alisisitiza Bw. Makufwe

Kwa upande wao, Viongozi na wananchi wa Kijiji hicho wamempongeza uwepo wa mpango huo kwani utafungua fursa mbalimbali na kuahidi kulinda maeneo yaliyotengwa hususani vyanzo vya maji kwa kutambua kuwa vyanzo hivyo ni muhimu kwenye mradi wa kimkakati wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.

“Mpango huu tumeupokea kwa mikono miwili, tumeweza kuainisha maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile malisho, misitu, na kwa upande wa vyanzo vya maji, tumeweka mikakati ya kuvisimamia kwa kuzuia shughuli ambazo si rafiki na vyanzo hivyo ili visikauke” alisema Bw. Godwin Konga, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpangala

Mtaalamu kutoka Tume ameeleza kuwa, mara baada ya kukamilika kwa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, hatua itakayofuata ni upimaji wa maeneo hususani mashamba ili kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za kimila.

“Kwa sasa ndio tunahitimisha zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vyote 44, baada ya hapo sasa tunaingia kwenye upimaji wa vipande vya ardhi katika mashamba ili mwananchi mmoja mmoja apate hati ya kumiliki ardhi” alisema Bw. Emmanuel Mabula, Mpima Ardhi kutoka Tume.

Kazi kama hiyo inafanyika katika Halmashauri nyingine tano (5) za Iramba, Bunda, Meatu, Itilima na Busega ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi nchini katika Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na Miradi ya Kimkakati na kutatua migogoro ya ardhi.