Habari

Mamlaka za Upangaji Matumizi ya Ardhi zapigwa Msasa

Mamlaka za Upangaji Matumizi ya Ardhi zapigwa Msasa
Apr, 03 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imezijengea uwezo Halmashauri za Wilaya za Meatu, Itilima na Busega kwa kuendesha mafunzo ya namna ya kuandaa, kusimamia na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi.

Ufanyikaji wa mafunzo hayo ni hatua ya awali ya zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji katika Halmashauri hizo ambayo itakayopelekea wananchi kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na baadae kupatiwa hatimiliki za kimila.

Aidha, mafunzo hayo yamefanyika kwa Timu za Usimamizi Matumizi ya Ardhi za Wilaya (PLUM Team) ambao uhusika moja kwa moja na uandaaji na kusimamia utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ngazi ya Wilaya.

Vilevile, mafunzo kuhusu Sheria za Ardhi, Mazingira na Maliasili yamefanyika katika ngazi za Vijiji ambapo kutokana na elimu wanayoipata, inawawezesha kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vyao. Aidha, Kamati za Usimamizi Matumizi ya Ardhi (VLUM) pamoja na Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji (VLC) na wananchi kwa ujumla wamepatiwa elimu hiyo.

Katika awamu ya kwanza, jumla ya vijiji 25 vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi, kupimwa mipaka kwa vijiji ambavyo vimebainika kutokuwa na mipaka kutokana na kugawanyika kwa vijiji hivyo. Vilevile, mara baada ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, vijiji hivyo vitaandaliwa Mipango Kina kwa ajili ya wananchi kumilikishwa ardhi.

Vijiji vinavyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ni Mwanyahina, Mganza, Sapa, Jinamo, Makao, Mwangudo, Iramba Ndogo, Shushuni, Mwabagimu, Mbushi, Sungu na Lukale.

Aidha, katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, vijiji vinavyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ni Longolambogo, Shishani, Mbogo, Mwamakili, Pijulu, Nyantugutu, Lung’wa, Nding’ho na Ngw’alali. Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, vijiji vinavyohusika kwenye zoezi hili ni Lukungu, Mwabayanda, Mwakiloba na Kijereshi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ina wajibu wa kuzijengea uwezo kuhusu upangaji, usimamzi na utekelezaji wa matumizi ya ardhi Mamlaka za Upangaji zote nchini.

Mkurugenzi Msaidizi Utafiti na Maendeleo kutoka Tume Dkt. Elimerinda Faustine (aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa Kikao Kazi kati ya Wataalamu wa Tume na Timu ya PLUM ya Meatu

Afisa Ardhi Mwandamizi Bw. Otmary Komba akiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Timu ya PLUM kuhusu uandaaji, usimamzi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi

Afisa Mipango Miji Mkuu Bw. Christopher Kazeri akiendesha Mafunzo kuhusu Sheria za Ardhi, kwa Halmashauri ya Kijiji cha Makao, VLUM pamoja na Baraza la Ardhi la Kijiji.

Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwangudo (mwenye kofia) akichangia mada wakati wa mafunzo ya uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji hicho.

Afisa Mifugo kutoka Tume Bw. Bwahama Bagenyi (aliyesimama) akiongea na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Iramba Ndogo, VLUM na Baraza la Ardhi la Kijiji wakati wa zoezi la uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi wa kijiji hicho.