Habari
Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 15 Kulinda Mazingira ya Ziwa Nyasa Yakamilika

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imekamilisha uwezeshaji wa kuandaa mipango ya matumizi ya vijiji kumi na tano (15) kwa ajili ya kulinda mazingira na vidakio (catchments) vinavyozunguka Ziwa Nyasa katika Wilaya za Ludewa, Makete, Mbinga, Nyasa na Kyela chini ya mradi wa Matumizi Endelevu ya Ardhi – Kidakio cha Ziwa Nyasa (Sustainable Land Management – Lake Nyasa Catchments).
Kazi hiyo iliyoanza Oktoba 2018 iliyohusisha utoaji elimu kuhusu maliasili na mazingira, ili kuisaidia jamii inayozunguka maeneo ya vidakio vya Ziwa Nyasa kutunza mazingira hasa baada ya kugundulika kuwa, shughuli nyingi za kibanadamu na zisizo rafiki kwa mazingira zinasababisha uharibifu wa vyanzo vya maji na kupelekea kina cha Ziwa kupungua na kutishia uwepo wa Ziwa hilo kwa miaka ijayo.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kazi hiyo, kiongozi wa timu iliyotekeleza kazi hiyo Bwana Eugen Cyrilo, amesema kuwa utekelezaji wa kazi zilizopangwa umeenda vizuri kwa mafanikio makubwa na malengo yaliyotarajiwa yamefikiwa. Hata hivyo alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa ambazo kwa namna moja au nyingine zilifanya kazi kuchelewa kwa muda.
“Tumefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi endelevu ya ardhi yatakayosaidia utunzaji wa mazingira na maliasili na namna gani wanaweza kunufaika kupitia uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya kukuza kipato, kuhifadhi vyanzo vya maji. Kwa ujumla muitikio wa wananchi ulikuwa ni mkubwa na kwamba elimu hiyo imewafikia wakati muafaka”. Alisisitiza Bw. Cyrilo
Hata hivyo, utatuzi wa migogoro ya mipaka kwa baadhi ya vijiji vilivyohusika na zoezi hilo na vile vya jirani ni moja ya changamoto kubwa ambayo timu ilikutana nayo. Aidha, changamoto hiyo iliifanya timu kujipanga upya ikiwa uwandani na kuhakikisha inatatua migogoro yote ya mipaka katika vijiji husika ili kuwezesha jamii za maeneo hayo kuandaa na baadae kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi bila vikwanzo vyovyote.
“Changamoto kubwa tuliyokutana nayo ni moja tu, katika Wilaya 4 kati ya 5 za mradi tulikuta mipaka ya baadhi ya vijiji haijakaa sawa, hivyo ilibidi tufanye kazi ya ziada ya kutatua migogoro hiyo ili kuhakikisha kazi inayofanyika inafuata Sheria pamoja na miongozo ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi” alisema Bw. Cyrilo
Vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi chini ya mradi huo uliofadhiliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (VPO) – Mazingira ni Ntumbati, Kipangala na Mkongobaki vilivyopo Wilaya ya Ludewa; pamoja na Utengule, Ugabwa na Kisasatu vilivyopo katika Wilaya ya Makete. Vijiji vingine vilivyonufaika na mradi ni Mtupale, Lundo na Kihuru vilivyopo katika Wilaya ya Nyasa; Kasumulu, Itete na Lugombo vilivyopo kwenye Wilaya ya Kyela; na vijiji vya Paradiso, Mkombozi na Ntanduwaro katika Wilaya ya Mbinga.