Habari

NLUPC, TFS Kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 100

NLUPC, TFS Kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 100
Feb, 01 2019

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameanza kazi za kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji takribani 100 vinavyozunguka hifadhi za misitu Tanzania.

Wakizungumza kwenye mkutano wa kusaini makubaliano kati ya taasisi hizo mbili, juu ya utekelezaji wa kazi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC Dkt. Stephen Nindi pamoja na Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa. Dos Santos Silayo wamesema kuwa malengo makuu ya zoezi hilo ni kuhifadhi misitu pamoja na kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

“Upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo haya yanayozunguka hifadhi za misitu nchini ni njia bora ya kuondoa migogoro kati ya wananchi na wahifadhi wa misitu na kuwasaidia wananchi kuangalia namna gani ya kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi”, alisema Dkt. Nindi.

Naye Mtendaji Mkuu wa TFS amesema kuwa zoezi hilo litasaidia kukabiliana na changamoto za uvamizi wa misitu kwani litawezesha wananchi wananchi wanaoishi kwenye vijiji hivyo kupanga Matumizi bora ya Ardhi kwenye vijiji vyao jambo ambalo litapunguza uvamizi kwenye misitu ya hifadhi.

“Mipango ya matumizi bora ya ardhi itawafanya wananchi wapunguze kilimo cha kuhama hama ambacho kwa kiasi kikubwa huchangia kupunguza maeneo ya misitu ya hifadhi, itawezesha wananchi kufanya shughuli zilizo rafiki na misitu pembezoni mwa hifadhi na hivyo kusaidia kutunza misitu hiyo”, alisisistiza Profesa Silayo

Zoezi hilo litaanzia kwenye vijiji ambavyo havijaandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, na kwa mwaka huu wa fedha vijiji taribani 60 vitawezeshwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kutumia wataalamu kutoka Tume, TFS, Wilayani pamoja na Halmashauri ya vijiji husika na wananchi wao.

Hatua hii imekuja baada ya kubainika kuwa misitu ya hifadhi inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazotishia uharibifu unaopelekea kupungua kwa uwezo wake kutoa huduma za kiekolojia na kijamii kutokana na uvamizi mkubwa wa maeneo ya misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho ya mifugo, uchimbaji wa madini, makazi na ukataji haramu wa miti kwa ajili ya nishati, mbao na nguzo za ujenzi.

Kwa kuzingatia hilo, TFS kwa kushirikiana na NLUPC imeona ni muhimu kuandaa mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi ambapo maeneo yote ya vijiji vinavyozunguka misitu ya hifadhi yatatengwa kwa shughuli mbalimbali ili kuhakikisha misitu inalindwa na kuhifadhiwa ambapo kazi hiyo tayari imeanza kwa vijiji 11 vilivyopo Lindi na Mtwara.