Habari

Ofisi ya Makamu wa Rais, Tume Kulinda Vyanzo vya Maji Ziwa Nyasa

Ofisi ya Makamu wa Rais, Tume Kulinda Vyanzo vya Maji Ziwa Nyasa
Oct, 09 2018

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (VPO) – Mazingira imeanza kazi ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji kumi na tano (15) kwa ajili ya kulinda mazingira na vidakio (catchments) vinavyozunguka Ziwa Nyasa katika Wilaya za Ludewa, Makete, Mbinga, Nyasa na Kyela. Kazi hiyo iliyoanza kwenye vijiji vya Ntumbati, Kipangala na Mkongobaki Wilayani Ludewa inatarajia kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu Sheria za ardhi, maliasili pamoja na upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo ndio chachu ya uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Akizungumza juu ya mradi huo, Mratibu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Eugen Cyrilo amesema kuwa mradi huu unalenga kuhifadhi mazingira hususani vyanzo vya maji ambavyo vinatiririsha maji kuingia Ziwa Nyasa. Hivyo basi mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji hivyo italenga katika kubainisha vyanzo vya maji na kutambua shughuli zinazofanyika maeneo ya vyanzo vya maji ili kuweka mikakati ya matumizi endelevu ya ardhi katika vijiji hivyo.

Aidha, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji hivi utasaidia kuboresha hali ya kiuchumi kwa jamii pamoja na uhifadhi wa mazingira na maliasili nyingine kama vile misitu na maji. Vijiji vingine vitakavyonufaika na mradi huu ni Mtupale, Lundu na Lituhi vilivyopo katika Wilaya ya Nyasa; Kasumuro, Itete na Ikombe vilivyopo kwenye Wilaya ya Kyela; Paradiso, Ruanda na Ntanduwaro katika Wilaya ya Mbinga; na vijiji vya Kisasatu, Ugabwa na Utengule katika Wilaya ya Makete.