Habari

​Tume Yaendesha Warsha Vyuo Vya Ardhi Kuhusu Dhana ya Ushirikishwaji Katika Upangaji wa Matumizi ya Ardhi

​Tume Yaendesha Warsha Vyuo Vya Ardhi Kuhusu Dhana ya Ushirikishwaji Katika Upangaji wa Matumizi ya Ardhi
Feb, 11 2019

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Lantmateriet ya nchini Sweden kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweeden (SIDA) imeendesha warsha katika Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es Salaam tarehe 6 Februari, 2019 na Chuo cha Ardhi mjini Morogoro tarehe 7 Februari, 2019. Warsha hizi zilihusu ushirikishwaji wa wananchi hasa makundi maalum katika upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.

Katika warsha iliyofanyika Chuo Kikuu Ardhi na kuhudhuriwa na Wakufunzi pamoja na Wanafunzi wa chuo hicho, wawezeshaji walikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume Dkt. Stephen Nindi; Bw. Kent Nillson kutoka Taasisi ya Lantmateriet na Bi. Lilian Looloitai kutoka Shirika Lisilo la Kiserikali la CORDS ambalo hufanya kazi zake katika Wilaya za Monduli na Longido Mkoani Arusha.

Akitoa mada katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume alielezea namna gani Sheria, na miongozo mbalimbali inayohusu upangaji wa matumzi ya ardhi inavyotambua na kuhimiza ushirikishwaji wa wananchi na kutaja makandi maalum kama vile wanawake kupewa kipaumbele katika hatua zote za upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi. Pia, Dkt. Nindi alitolea mfano wa Mwongozo Shirikishi wa Upangaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji (Participatory Land Use Management Guidelines) ambao umetamka bayana juu ya uundwaji wa kamati za upangaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi za vijiji kuwa lazima ziwe na wajumbe wanawake wasiopungua watatu.

Wakielezea uzoefu wao juu ya ushirikishwaji katika upangaji wa matumizi ya ardhi, Bw. Kent Nillson kutoka Taasisi ya Lantmateriet amesema kuwa Sweden ilianza kupangwa toka mwaka 1692 ambapo hadi hivi sasa ushiriki wa wananchi katika shughuli za upangaji na umiliki wa ardhi umeimarika kwa kiasi kikubwa.

Na kwa upande wa mwezeshaji kutoka Asasi ya Kiraia ya CORDS, Bi. Lilian Looloitai amesema kuwa, kwa muda mrefu sasa CORDS wamejikita katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Monduli ambapo ushiriki wa wanawake katika zoezi hilo unaonyesha kufanikiwa. Bi. Lilian amesema kuwa kwa sasa kumekuwepo na ongezeko la idadi ya wanawake wanaoshiriki na kutoa maoni katika mikutano ya kijiji pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Warsha kama hii pia imefanyika Chuo cha Ardhi mjini Morogoro ambapo imekuwa chachu ya majadiliano juu ya upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa njia ya ushirikishwaji pamoja na kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya kusimamia sekta ya ardhi kwa kuzingatia masilahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.