Habari

Vijiji 12 Meatu vyakamilisha Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Vijiji 12 Meatu vyakamilisha Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi
Apr, 15 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imekamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 12 vinavyopakana na Pori Tengefu la Maswa pamoja na vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi Wanyamapori ya Makao (Makao WMA) ili kuhakikisha rasilimali hizo zinanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.

Zoezi hilo limefanyika kwa kuwawezesha wananchi kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali hatua itakayowasaidia kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi pamoja na kuwasidia kupata hatimiliki za ardhi.

Wakizungumza wakati wa kuwasilisha rasimu za mipango hiyo kwenye Mikutano ya Vijiji kwa ajili ya kuidhinishwa, baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuandaa mipango hiyo ambayo itawafanya kuondokana na muingiliano wa matumizi ya ardhi kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi vijijini mwao.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea mpango huu wenye faida, kwani tumeweza kupata elimu kuhusu masuala ya ardhi pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali, kwa sisi wananchi itatusaidia kutokuwa na migogoro kati yetu” alisema Bw. Timotheo Ngasa, Mkazi wa Kijiji cha Sapa.

Kwa upande wake, Alphayo Kabati, mkazi wa kijiji cha Makao ameeleza kuwa zoezi hilo limekuwa na manufaa kwa wananchi na limewafurahisha kwa kuwa limesaidia mgawanyo wa maeneo kulingana na shughuli tofauti tofauti.

“Zoezi hili lilipoanza wawezeshaji walifika hapa kijijini wakatuelimisha na baadae tukaanza kupanga maeneo muhimu ambapo tulitenga maeneo ya kilimo, machungio, huduma za jamii na maeneo mengineyo na mwisho tuliitisha mkutano wa wananchi wote na kuhakikisha kila mwanakijiji anaelewa kuhusu mpango wa matumizi ya ardhi” alisema Bw. Kabati.

Kukamilika kwa zoezi hilo kunapisha hatua nyingine ya upangaji matumizi ya ardhi ambapo itaandaliwa Mipango Kina (Detail Land Use Plans) ambayo itawezesha mwananchi mmoja mmoja katika vijiji hivyo watapimiwa maeneo yao na kumilikishwa kupitia Hatimiliki za Kimila.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi hilo, Kiongozi wa Timu ya Wataalamu waliowezesha zoezi hilo kwa Wilaya ya Meatu, Bw. Amos Mpuga ameeleza kuwa wamefanikiwa kuvifikia vijiji vyote 12 na mchakato utakaofuata ni kwa ajili ya kutoa Hati miliki kwa wananchi wa vijiji hivyo.

“Kwa sasa, tunahitimisha hili zoezi, kinachofuata ni kuandaa Mipango Kina, kwa hiyo Tume kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya, tutakuja tena awamu ya pili kuandaa Mipango Kina ambayo itawawezesha wananchi kupimiwa vipande vyao vya ardhi na kupatiwa hatimiliki za kimila ambazo zitawafanya kuwa na milki salama na kuwakwamua kiuchumi” alisema Bw. Mpuga.

Uandaaji wa mipango hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha vijiji vyote vilivyopo pembezoni mwa Hifadhi vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuepuka muingiliano wa matumizi ya ardhi kati ya hifadhi na wananchi waishio kwenye vijiji hivyo.

Mjumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji cha Jinamo (VLUM) akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa matumizi ya ardhi wa kijiji kwa Halmashauri ya Kijiji hicho.

Mjumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji (aliyesimama) akiwasilisha rasimu ya mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji kwenye mkutano mkuu wa Kijiji cha Sapa

Wapima Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu wakipima mipaka ya Vijiji mara baada ya wananchi kukubaliana mipaka yao wakati wa zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 12 Wilayani Meatu

Wapima ardhi kutoka Tume wakiwaongoza wajumbe wa Vijiji vya Mwangudo na Iramba Ndogo kusimika alama ya mpaka (Beacon) inayotenganisha vijiji hivyo mara baada ya kumaliza mgogoro wa mpaka baina ya vijiji hivyo

Sehemu ya Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Jinamo wakiwa kwenye mkutano mkuu wa Kijiji kwa ajili ya kujadili na kupitisha mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji hicho.

Afisa Mifugo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Hamisa Mchomvu akitoa elimu ya upangaji matumizi ya ardhi katika mkutano mkuu wa Kijiji cha Sapa wakati wa kuwasilisha mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji hicho

Mpima Ardhi kutoka Tume (Katikati) Bw. Mikidadi Kalimang’asi akiwaongoza wajumbe kutoka vijiji vya Mbushi na Jinamo kwenye kikao cha kujadili mpaka unaowagawanyisha Vijiji hivyo

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sungu Bw. Amos Mukama (Katikati) akisaini nyaraka za makubaliano ya mpaka kati ya Kijiji cha Sungu na Iramba Ndogo mara baada ya kukamilika kwa upimaji wa mpaka unaogawanyisha Vijiji hivyo

Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mh. Fauzia H. Ngatumbura (Katikati) akipokea mrejesho kutoka kwa wataalamu wa Tume na Halmashauri ya Wilaya mara baada ya kukamilika kwa kazi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 12 katika Wilaya hiyo.