Habari
Vijiji 164 katika Mikoa 7 kupangiwa Matumizi ya Ardhi
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeanza zoezi la kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 164 vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya 10 kwenye Mikoa 7 nchini.
Uandaaji wa mipango hiyo unalenga kwenye Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na miradi ya Kitaifa ya Kimkakati ikiwemo Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Aidha, mbali na Vijiji vilivyopo kwenye miradi hiyo, Vijiji vingine vitakavyowezeshwa kuandaa mipango hiyo ni vilivyopo kwenye Wilaya za mipakani na nchi jirani pamoja na Vijiji vilivyokuwa na migogoro na maeneo ya Hifadhi ambavyo vilitolewa maamuzi na Mawaziri 8 wa kisekta.
Akiongea Jijini Dodoma na wataalamu wa Tume wanaokwenda kuwezesha kazi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Profesa Wakuru Magigi amewataka wataalamu hao kuzitendea haki taaluma zao wakati wote wa utekelezaji wa kazi hiyo na kutanguliza mbele maslahi ya wananchi.
“Serikali hii inayoongozwa na Mh. Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo tunavyokwenda huko tukahakikishe tunaowahudumia wananchi wale kikamilifu kwa kuwawezesha kupanga matumizi ya ardhi zao, tukafanye kazi kwa bidii na kwa umakini mkubwa kuhakikisha tunaleta matokeo tarajiwa” alisema Prof. Magigi
Halmashauri za Wilaya zitakazohusika na zoezi hili ni Kwimba na Misungwi mkoani Mwanza, Kishapu na Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga, Igunga na Uyui katika mkoa wa Tabora. Aidha, Halmashauri nyingine ni Tarime mkoani Mara, Meatu mkoani Simiyu, Korogwe mkoani Tanga pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe iliyopo mkoani Kigoma.
Uandaaji wa mipango hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project) unatekelezwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo.
Vilevile, uandaaji wa mipango hiyo ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo (2021/22 – 2025/26) unaotaka asilimia 50 ya vijiji vyote nchini viwe vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Aidha, ufanyikaji wa kazi hii pia ni utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya viongozi wa Serikali kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi, kulinda uhifadhi pamoja na kuhakikisha wananchi wanakuwa na milki salama za ardhi zao.