Habari

Vijiji 364 Vyaandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Mwaka wa Fedha 2018/19

Vijiji 364 Vyaandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Mwaka wa Fedha 2018/19
Sep, 24 2019

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imepiga hatua kubwa katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi nchini kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo imefanikiwa kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 364 kulinganisha na vijiji 250 vilivyotegemewa kuandaliwa mipango hiyo katika mwaka wa fedha 2018/19.

Uwezeshaji wa kuandaa mipango hii umefanikishwa na Serikali kupitia fedha zake za ndani za miradi ya maendeleo pamoja na ushirikiano wa Taasisi nyingine za Serikali, Asasi za Kiraia na Mashirika mengine ya kimaendeleo. Upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo umewezesha kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 102 katika Wilaya 13 pamoja na kuandaa mipango kina kwenye maeneo 9 ya miji midogo.

Mipango hiyo ya matumizi ya ardhi imefanyika katika Wilaya ambazo vijiji vyake vinapitiwa na mradi wa bomba la mafuta (EACOP) kwa upande Tanzania. Wilaya hizo ni Misenyi, Bukoba, Muleba, Chato, Mbogwe, Bukombe, Igunga, Iramba, Singida, Kiteto, Chemba, Handeni na Muheza. Maeneo yaliyowezeshwa kuandaliwa mipango kina ikiwa ni pamoja na kuandaa michoro ya Mipangomiji ni vitovu vya vijiji ambavyo vina viashiria vya ukuaji kuelekea kuwa miji midogo na vitovu vya vijiji vilivyoiva katika Wilaya za Igunga, Singida na Bukombe.

Kazi hii inatekelezwa chini ya mradi wa upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi unaolenga maeneo makuu matatu ya utekelezaji ambayo ni vijiji vinavyopitiwa na bomba la mafuta vilivyopo katika Wilaya 24, vijiji vilivyopo mipakani na nchi jirani pamoja na vijiji vilivyopo katika Wilaya zilizokuwa na kambi za wakimbizi za Mishamo, Katumba na Ulyankulu katika Wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu pia imefanyika tathmini ya matumizi ya ardhi na mazingira katika maeneo zilipokuwepo kambi za wakimbizi hivyo kazi iliyobakia ni kuviwezesha vijiji husika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi.

Katika hatua nyingine, kufikiwa kwa idadi hiyo kubwa ya vijiji vilivyoandaliwa mipango pia imewezeshwa na jitihada za wadau wa ndani na nje ya Serikali kwa ajili ya kulinda maliasili za nchi zinazozunguka vijiji mbalimbali. Kwa upande wa mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira kwa kushirikiana na Tume imewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 30 katika Wilaya 9 kwa ajili kulinda vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji Ziwa Nyasa pamoja na kudhibiti uharibifu wa ardhi na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ili kukabiliana na upungufu wa chakula.

Wakati huo huo, Tume kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) imewezesha kuandaliwa kwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 74 vinavyopakana na hifadhi za Taifa za wanyamapori katika Wilaya za Bariadi, Bunda, Karatu, Kondoa, Mbulu, Simanjiro na Tarime. Kazi hii ambayo bado inaendelea, ina lengo la kumaliza migogoro yote iliyopo kati ya hifadhi za wanyamapori na vijiji jirani ikiwa na lengo la kuvifikia vijiji vyote nchini vilivyopakana na hifadhi vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya 390.

Kazi hii pia inaambatana na upimaji wa maeneo mbalimbali ya makazi na mashamba pamoja na utoaji wa hati miliki za kimila 25 za mfano kwa kila kijiji ili Halmashauri za Wilaya husika ziendelee kumilikisha ardhi zilizopangwa kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande mwingine, ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na uhifadhi endelevu wa misitu nchini, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Tume imewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 60 vinavyopakana na misitu ya hifadhi. Upangaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji hivi umesaidia kuelimisha wananchi na kuwashauri kufanya shughuli ambazo ni rafiki na misitu ili kuthibiti uharibifu wa misitu ambao unatokana na uvamizi wa mara kwa mara wa maeneo hayo.

Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji hivyo umefanyika katika Wilaya 17 za Muheza, Mbeya, Morogoro, Kilindi, Biharamulo, Geita, Bahi, Chemba, Nanyumbu na Chamwino. Wilaya nyingine ni pamoja na Kasulu, Urambo, Chalinze, Lindi, Kilwa, Mbarali na Masasi. Kazi hii bado inaendelea na inalenga kuvifikia jumla ya vijiji 270 katika kipindi cha miaka mitatu.

Ukiachilia mbali uwezeshwaji huo mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na Taasisi zake, vijiji vingine takribani 100 vimewezeshwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na program na wadau kutoka Asasi za Kiraia pamoja na Mashirika ya imaendeleo ya ndani na nje ya nchi (kama vile Programu ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi – LTSP, Programu ya LIC na PFP, Ushirika wa Taasisi za WWF na CARE, Taasisi za SOLIDARIDAD, TNC, UCRT, OIKOS East Africa na Shirika la OXFAM) ambapo inafanya idadi ya vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 kuwa 364.

Kazi hizi zimehusisha utoaji elimu kwa umma juu ya Sheria na miongozo ya ardhi, usimamizi wa maliasili na mazingira pamoja na kujengea uwezo timu za upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi za Wilaya, Vijiji pamoja na Mabaraza ya ardhi ya vijiji kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi vijijini. Sambamba na hayo, kazi hizo zimeambatana na uhakiki wa mipaka kati ya vijiji na vijiji, vijiji na hifadhi na kutatua migogoro iliyobainika na hatimaye kuandaa vyeti vipya vya ardhi ya vijiji.