Habari

Vijiji katika Mikoa 10, Halmashauri 15 kunufaika na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji

Vijiji katika Mikoa 10, Halmashauri 15 kunufaika na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji
Oct, 17 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 15, katika Mikoa 10 nchini, inatarajia kuanza kazi ya uwezeshaji wa kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 286, ikiwa ni jitihada za Serikali katika kuhakikisha kunakuwa na matumizi ya ardhi endelevu, kuepusha migogoro, kulinda uhifadhi pamoja na kuwahakikishia wananchi milki salama za ardhi zao.

Akizungumza na wataalamu wa Tume wanaokwenda kuwezesha kazi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Prof. Wakuru Magigi, amewataka wataalamu hao kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na kuhakikisha maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla yanazingatiwa.

“Ukitumwa kazi lazma uhakikishe unaifanya kwa kuzingatia utaalamu wako, wananchi wanatutegemea tukawasaidie kuandaa hii mipango, lakini pia lazma tufanye kazi ili kuhakikisha malengo ya Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kutekeleza maagizo na maelekezo ya Viongozi wetu” alisema Prof. Magigi

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa idadi kubwa ya Vijiji vinavyoandaliwa mipango ya matumizi ya inatokana na utekelezaji wa Miradi miwili ya maendeleo inayotekelezwa na Tume kupitia fedha na maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mradi wa kwanza ni ule wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project). Utekelezaji wa Mradi huu unalenga Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati kama vile Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere (JNHPP).

Maeneo mengine yanayohusika na Mradi huo ni Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kimataifa (SGR), Wilaya na Vijiji vilivyopo mipakani na nchi jirani pamoja na Vijiji vyenye migogoro kutokana na maelekezo ya Baraza la Mawaziri

Vilevile, ufanyikaji wa kazi hii utajumuisha utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi, Kikanda, Wilaya na Vijiji utakaowezesha upatikanaji kwa maeneo ya uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya viwanda nchini kwa kutumia ubunifu wa kidijitali (ZORED). Aidha, upangaji matumizi ya ardhi kupitia Mradi huu utajikita katika maeneo yatakayowezesha kuwa na uazalishaji wa mazao ya kilimo yenye tija yatakayochakatwa kupitia viwanda vitakavyoanzishwa.

“Mnatawanyika katika Halmashauri 15, kila eneo lina lengo lake la kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, mkawezeshe uandaaji wa mipango hii kwa kuzingatia malengo ya Mradi husika. Kuna Halmashauri zinazopitiwa na Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati, lakini pia kuna Vijiji ambapo yanatakiwa yaainishwe maeneo ya uwekezaji ili kufanya uazalishaji mazao wenye tija kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya viwanda” alisisitiza Prof. Magigi.

Vilevile, Mkurugenzi Mkuu aliwakumbusha wataalamu hao kuwa jukumu kubwa walilonalo kwenye kazi hiyo itakayoifanyika kwa kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba 2023 ni kuhakikisha wanawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi itakayokuwa na tija kwa wananchi kwa kuwahakikishia milki salama za ardhi zao, kuangalia namna gani mipango hiyo inavyoweza kuimarisha uhifadhi pamoja na kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi.

Halmashauri za Wilaya zitakazowezeshwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ni Musoma, Bunda, Butiama na Rorya zilizopo katika Mkoa wa Mara, Makete na Ludewa zilizopo katika Mkoa wa Njombe pamoja na Shinyanga na Ushetu zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Halmashauri nyingine ni Ruangwa katika Mkoa wa Lindi, Tunduru mkoani Ruvuma, Igunga katika Mkoa wa Tabora, Sumbawanga mkoani Rukwa, Magu katika Mkoa wa Mwanza, Korogwe mkoani Tanga pamoja na Halmashuri ya Wilaya ya Singida iliyopo katika Mkoa wa Singida.

Wataalamu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Tume Prof. Wakuru Magigi (aliyesimama) akitoa maelekezo juu ya utekelezaji wa kazi ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 286.

Msafara wa Wataalamu wa Tume wakijiandaa kuondoka Jijini Dodoma kuelekea katika Halmashauri za Wilaya 15, katika Mikoa 10 kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 286.