Habari
Waziri Lukuvi Azindua Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amezindua rasmi Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi (Land Use Planning Project) utakaohusisha Wilaya 38 na Vijiji 1502 vitakavyopitiwa na Bomba la Mafuta la Africa Mashariki (EACOP) kutoka Mutukula-Kagera hadi Chongoleani-Tanga; Wilaya na Vijiji vilivyokuwa na kambi za wakimbizi za Ulyanhulu, Mishamo na Katumba pamoja na Wilaya na Vijiji vilivyopo mpakani mwa Tanznia na nchi jirani.
Akihutubia mamia ya wananchi wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Lukuvi amesema kuwa upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ambayo imeweka misingi ya ushirikishaji wa wadau wote ili kuhakikisha kunakuwepo na matumizi ya ardhi yenye tija kwa wananchi ambayo yatahakikisha rasilimali zilizopo juu ya ardhi zinatumika vizuri kuondoa matumizi kinzani yatakayoepusha migogoro ya ardhi, kuimarisha umiliki na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo na kilimo.
“Upangaji wa matumizi ya ardhi nchini unasimamiwa na Sheria ya Upangaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007 ambayo inasisitiza na kuweka malengo ya kuwezesha wamiliki wa ardhi kutumia kwa ufanisi na uzalishaji zaidi” alisema Mhe. Lukuvi na kuongeza kuwa “lazima kuwezesha na kuasisi mfumo wa kuzuia migogoro ya matumizi ya ardhi na kufanya tathmini ya matumizi ya ardhi yaliyopo na yanayopendekezwa sambamba na Sera za Serikali kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo usimamizi endelevu wa matumizi ya ardhi nchini.”
Pia Mheshimiwa Lukuvi alibainisha na kusisitiza kuwa utekelezaji wa Mradi huu wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015 – 2020, Ibara ya 37 Kipengele (b) ambacho kinaelekeza juu ya upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kuanzia ngazi ya Taifa, Wilaya na Vijiji. Hivyo kupitia Mradi huu, ambapo vijiji na Wilaya nyingi zitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi , itahusisha pia uandaaji na kuhuisha michoro ya mipango miji katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 2018 hadi Juni 2021.
Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi utawezesha wananchi kuweka utaratibu wa matumizi bora ya rasilimali za ardhi, kutatua migogoro ya ardhi, kuimarisha miliki za ardhi, kuboresha matumizi na hifadhi ya ardhi kulingana na mapendekezo na uwezo wa walengwa. Hivyo Mhe. Lukuvi alisisitiza juu ya umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kupanga ardhi yao kwani mipango hii ya matumizi ya ardhi inatoa mchango mahususi katika maendeleo vijijini na nyenzo muhimu katika kuboresha hali ya maisha ya watu, kuongeza ushalishaji, kuondoa umaskini na kuhifadhi mazingira.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Dkt. Stephen Nindi amesema awamu ya kwanza ya utekelezaji imeanza mwezi Aprili 2019 kwa kuhusisha jumla ya Wilaya 13 kati ya 19 zinazopitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) ambapo jumla ya vijiji 48 tayari vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Wilaya zinazoguswa na Mradi wa Bomba la Mafuta ambako vijiji vyake vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ni Misenyi, Muleba, Bukoba, Chato, Geita, Mbogwe, Bukombe, Kahama Nzega, Iramba, Mkalama, Singida, Chemba, Kondoa, Kiteto, Hanang, Muheza, Handeni na Korogwe.
Aidha Dkt. Nindi amesema upangaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji vitakavyopitiwa na bomba la mafuta unaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi wa vijiji hivyo juu ya ardhi na maliasili pamoja na kuondokana na matumizi kinzani pembezoni mwa bomba ambayo yanaweza kusababisha athari za kijamii na mazingira.
Uzinduzi huo uliofanyika tarehe 25 Mei 2019 katika kijiji cha Sojo, Kata ya Igusule Wilayani Nzega pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu; Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Aggrey Mwanri pamoja na viongozi wengine wa Serikali ngazi ya Wilaya.