Habari
Wilaya za Tanganyika na Uvinza zaandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya za Uvinza Mkoani Kigoma na Tanganyika Mkoani Katavi imeratibu uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya (District Land Use Framework Plans - DLUFPs) ambayo itakuwa dira katika matumizi ya rasilimali ardhi kwa miaka 20 ijayo kwenye Wilaya hizo.
Mipango hiyo wa matumizi ya ardhi ya Wilaya imelenga katika kufanya tathmini ya rasilimali ardhi zilizopo kwenye Wilaya hizo na kupanga namna gani zinaweza kutumika kwa njia bora ili kuongeza uzalishaji mali, mapato la Wilaya, mwananchi mmoja mmoja; uhifadhi wa mazingira na maliasili.
Aidha, mipango hiyo imetambua rasilimali ardhi zilizopo na kuzipangia matumizi kwa mujibu wa uwezo wa rasilimali ardhi husika. Vilevile, kupitia maoni na taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali, mipango hiyo ya Wilaya imebainisha migogoro ya matumizi ya rasilimali ardhi na kuiwekea mikakati ya kuitatua kupitia upangaji wa matumizi ya ardhi uliokubalika baina ya watumiaji ardhi katika ngazi mbalimbali za Wilaya.
Mkurugenzi anayeshughulikia Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu kutoka Tume, Bw. Joseph J. Osena amewataka wadau kushirikiana katika kuandaa mipango hiyo ili utekelezaji wake uwe rahisi na itasaidia katika kuondoa migongano ya kimatumizi baina ya shughuli mbalimbali au Taasisi.
“Tukishirikiana tunaamini tutaweza kupunguza au kuondoa kabisa migogoro ya matumizi ya ardhi, ardhi hiyo mwingine atataka kuitumia kwa kilimo, malisho, uhifadhi, makazi au shughuli nyingine yeyote, mahitaji haya yanayokinzana kusipokuwa na mfumo mzuri unaokubalika na watumiaji wote, kunaweza kutokea migogoro ya matumizi ya ardhi ambayo inaweza kuathiri mtu mmoja mmoja au hadi Taasisi kwa Taasisi”, alisema Bw. Osena.
Aidha, Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya inagusa kila sekta, ndio maana kwenye kila hatua lazma ishirikishe wadau wote ili kukubaliana kwa pamoja utengaji wa maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile ukuwaji wa miji, maeneo ya malisho, uhifadhi wa misitu, shoroba za wanyamapori na mengineyo kwa mujibu wa Sheria na mahitaji ya wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye vikao kazi vya kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali katika Wilaya za Tanganyika na Uvinza, baadhi ya viongozi wa Wilaya na wadau wengine wamehimiza katika usimamizi wa mipango hiyo ili iwe mwarobaini wa changamoto za matumizi ya rasilimali ardhi zinazoikabili Wilaya hizo zenye utajiri mkubwa wa uoto wa asili, vyanzo vya maji na baadhi ya wanyamapori hadimu duniani.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mh. Hanafi Msabaha amewataka viongozi na watendaji kusimamia mpango unaoandaliwa kwa uaminifu ili kuleta tija na kuepuka kuleta migogoro baina ya wananchi. "Twendeni tukausimamie huu mpango, lakini tuwe waaminifu, tusiuze ardhi kiholela pasipo kufuata Sheria na taratibu zilizopo ili kuepuka kuwagombanisha wananchi, kama kuna ardhi inayotosha mifugo kadhaa, tusizidishe mifugo hiyo kuliko uwezo wa ardhi iliyopo, pale mifugo inapozidi, tuwaelimishe wananchi wetu kuvuna mifugo hiyo ili tuwe na mifugo inayoendana na ardhi tulionayo” alisema Mh. Msabaha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mh. Hamad Mapengo amekiri kuwa Wilaya ya Tanganyika inakumbwa na migogoro mingi ya matumizi ya ardhi na anaamini kuwa uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya unaenda kutatua changamoto hiyo.
Mwenyekiti huyo alisisitiza juu ya ushirikishwaji wa wadau wote kuanzia ngazi ya kijiji hadi Wilayani ili kurahisisha utekelezaji wa mpango huo. Vilevile, Mh. Mapengo alikazia suala la kuheshimu matumizi yaliyopangwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwani bila kufanya hivo mpango utakaoandaliwa hautotekelezeka.
Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumzi ya Ardhi imepewa mamlaka ya kuratibu uandaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini. Aidha, Halmashauri za Wilaya na Vijiji, kama mamlaka za upangaji, zimepewa mamlaka ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kusimamia utekelezaji wake.