Habari

Miradi ya Upangaji Matumizi ya Ardhi na Uhifadhi wa Misitu kunufaisha Vijiji 112

Miradi ya Upangaji Matumizi ya Ardhi na Uhifadhi wa Misitu kunufaisha Vijiji 112
Oct, 07 2024

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) inatarajia kuanza zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 112 vilivyopo kwenye Halmashauri za Wilaya 11 katika Mikoa 9 hapa nchini kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo na ushirikiano kati ya Tume na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS).

Kazi hiyo itakayofanyika kwa kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za Upangaji, inalenga katika kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi Vijiji katika Wilaya zinazopitiwa na Miradi ya Kimkakati inayotekelezwa na Serikali pamoja na Vijiji vinavyopakana na safu za misitu ya miombo kwa ajili ya kufanya uhifadhi endelevu.

Kati ya Vijiji hivyo, jumla ya Vijiji 98 Katika Wilaya zinazopitiwa na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere (JNHPP) pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) vitanufaika na uandaaji huo wa mipango ya matumizi ya ardhi.

Aidha, Vijiji vingine vitakavyoguswa na kazi hiyo ni Vijiji vilivyopo kwenye Wilaya za mipakanina nchi jirani pamoja na Vijiji vilivyokuwa na Migogoro ya matumizi ya ardhi ambavyo vilitolewa maamuzi na Serikali kati ya Vijiji 975 vilivyokuwa na migogoro na maeneo ya Hifadhi.

Halmashauri za Wilaya zitazowezeshwa kuandaa Mipango hiyo ya Vijiji ni Busokelo (Mbeya), Nyasa (Ruvuma), Nzega (Tabora), Mbogwe (Geita), Morogoro DC (Morogoro), Buhigwe (Kigoma), pamoja na Rombo mkoani Kilimanjaro.

Vilevile, kati ya Vijiji hivyo, jumla ya Vijiji 14 vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Urambo na Sikonge Mkoani Tabora pamoja na Wilaya ya Mlele mkoani Katavi vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuendeleza Uhifadhi wa Maliasili na utunzaji wa misitu ya miombo ambayo ipo hatarini kutoweka.

Uandaaji wa mipango hiyo ni utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project No. 4951) pamoja na Mradi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame Tanzania (Integrated Landscape Management in Dry Miombo Woodlands of Tanzania).