Habari
DC ataka uendelevu wa zoezi la Umilikishaji

DC ataka uendelevu wa zoezi la Umilikishaji
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mkoani Tanga Mheshimiwa William Mwakilema ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kutenga bajeti na kushirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza zoezi la upimaji na kumilikisha Wananchi vipande vyao vya ardhi ili kuondoa migogoro miongoni mwa watumiaji mbalimbali wa ardhi Vijiji.
Mkuu huyo wa Wilaya ameyasema hayo Juni 20, 2025 katika hafla wa uzinduzi wa ugawaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) zaidi ya 1,300 kwa Wananchi wa Vijiji vya Makumba na Mgila zilizoandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
“Niendelee kusisitiza kwa Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na wataalamu ulionao, tuendelee kushirikiana na kutenga bajeti kwa ajili ya mwendelezo wa zoezi hili, tukifanya hivi tutawawezesha wananchi wetu wafanye kazi za kwa amani pasipo misuguano ya hapa na pale ili wafanye shughuli za uzalishaji mali na kujiletea maendeleo” alisema Mhe. Mwakilema.
Akitoa maelezo ya awali katika hafla hiyo, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini kutoka Tume ambaye pia ndiyo msimamizi wa zoezi hilo, Bw. Amos Mpuga, alieleza kuwa uandaaji wa Hatimiliki hizo ni utekelezaji wa hatua ya tano (5) na sita (6) ya uandaaji wa Mipango ya matumizi ya ardhi zinazolenga kuandaa Mipango Kina (Detail land use plans) na kumilikisha ardhi.
Bwana Mpuga alisema kuwa, wataalamu kutoka Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe walipiga kambi katika Vijiji hivyo na kuwezesha kupima maeneo ya wananchi 1,307, ambapo kwa Kijiji cha Makumba, wananchi 672 wamenufaika na Hatimiliki hizo huku Wananchi 635 wamefikiwa kwa upande wa Kijiji cha Mgila.
Zoezi kama hilo limefanyika pia katika Halmashauri za Wilaya nyingine 4 za Ikungi, Mpimbwe, Kishapu na Ruangwa ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa upangaji Matumizi ya Ardhi (Land Use Planning Project) kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.