Habari
Uhifadhi kuleta neema kwa Wananchi Ikungi

Wananchi zaidi ya 1,000 wa Vijiji vitano vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida wanatarajiwa kuwezeshwa kumiliki ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) kwa lengo la kuimarisha Uhifadhi wa Mazingira, Kilimo endelevu pamoja na Usawa wa jamii katika usimamizi wa ardhi.
Utekelezaji wa kazi hiyo utahusisha kuleta matokeo ya Usimamizi bora wa Ardhi na kufanya jamii yenye Uwajibikaji hasa katika makundi ya wanawake kuwasaidia katika matumizi sawa ya rasilimali za asili ikiwemo Ardhi ya binafsi, Ardhi ya Kijiji, Ardhi ya misitu, mazao yasiyo ya miti na maji, pamoja na kuhakikisha wanawake wanashiriki katika usimamizi na kunufaika na rasilimali hizo.
Katika kufikia hilo, wataalamu watatoa elimu na kuwajengea uwezo wananchi kuhusu umiliki na usimamizi wa ardhi pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali ardhi za asili zilizopo Vijijini. Aidha, kazi hiyo inategemewa kuwezesha na kuhamasisha ushiriki hai na kutumia uwezo wa wanawake katika michakato ya maamuzi ngazi ya Vijiji.
Vilevile, kazi hiyo inatarajiwa kusaidia kuimarika kwa usalama wa umiliki wa ardhi kupitia matumizi madhubuti na jumuishi zaidi ya haki za Kimila za umiliki wa ardhi katika ngazi ya Kijiji, kuimarisha shughuli za Kilimo pamoja na usimamizi wa mazingira katika maeneo ya Vijiji.
Kufanyika kwa kazi hiyo ni utekelezaji wa Mradi wa UKIJANI unaolenga kuwawezesha wanawake kupitia fursa zaidi za kiuchumi, uelewa pamoja na ushiriki mkubwa, ikijumuisha uongozi katika maamuzi ya jamii, ili wawe na uwezo zaidi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchangia katika kuboresha maisha ya familia na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika.
Kazi hiyo inawezeshwa na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Shirika la HELVETAS linalotekelezwa Mradi huo pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Vijiji vitakavyo nufaika na kazi hiyo ni Mkunguakiendo, Mnane na Nkundi katika Kata ya Kikio, Kijiji cha Manang’ana katika Kata ya Sepuka pamoja na Kijiji cha Kipanda kilichopo Kata ya Mtunduru.