Habari
Wananchi Ruangwa wanufaika na Hatimiliki za Ardhi

Zaidi ya Wananchi 1200 wa Vijiji vya Nambilanje na Namkatila vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi wamemilikishwa vipande vya ardhi zao kisheria kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila zoezi lililowezeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Akiongoza zoezi la ugawaji wa Hatimiliki kwa wananchi wa Vijiji hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Frank Chonya alieleza umuhimu wa kutunza wa Hati hizo huku akibainisha kuwa nyaraka hizo ni muhimu kwa usalama wa milki uthibitisho wa uhalali wa matumizi ya ardhi.
“Tusiangalie Hati hizi kama karatasi tu, kwa maana hizi ni nyenzo za maendeleo, ni muhimu kwa kila mwananchi kwa maana zina manufaa kwa mfano ni muhimu kwa usalama wa umiliki wa mali na vilevile ni uthibitisho wa uhalali wa matumizi ya ardhi hivyo tuzitunze vizuri” alisisitiza Bw. Chonya.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa zoezi hilo limeleta suluhu kwa changamoto za muda mrefu za migogoro ya ardhi iliyohusisha wakulima na wafugaji, na kuishukuru Serikali kupitia Tume kwa kuona umuhimu wa upimaji maeneo na kuwamilikisha wananchi Wilayani humo.
Kwa upande wake msimamizi wa zoezi hilo kutokea Tume ambaye ndiye Mkuu wa Kanda Ya Kusini Bw. Baltazari Sumari amesema kuwa jumla ya Hati 643 zimetolewa kwa wananchi wa kijiji cha Nambilanje na zingine 600 zimetolewa kwa wananchi wa kijiji cha Namkatila.
Utoaji wa Hati hizo unakuja mara baada ya Vijiji hivyo kuwezeshwa kuandaaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo ni mojawa wapo ya sifa inayopelekea wananchi wa Vijiji husika kumilikishwa ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Ardhi ya Vijiji Sura 114.