Habari

Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Mkoa wa Shinyanga yawasilishwa kwa Wadau

Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Mkoa wa Shinyanga yawasilishwa kwa Wadau
Sep, 09 2024

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imewasilisha Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Regional Land Use Framework – SRLUFP) kwa wadau wanaohusika na matumizi ya ardhi Mkoani humo zikiwemo Taasisi za Serikali, Halmashauri (Wilaya, Mji na Manispaa), Wawekezaji, pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yaliyopo Mkoani humo.

Akufungua Mkutano huo uliofanyika tarehe 05/09/2024 mjini Shinyanga, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anamringi Macha amewataka wadau hao kujadili kwa makini rasimu ya mpango huo na kusisitiza majadiliano yanayolenga kuheshimu mgawanyo wa matumizi ya ardhi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ili kujiletea maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Macha amesema kuwa japokuwa Shinyanga ina migogoro midogo midogo ya ardhi kati ya Wakulima na wafugaji na ili kuzuia migogoro hiyo isiwe mikubwani muhimu kila ardhi iheshimiwe kwa kadri ya ilivyotengwa kama ni ya kilimo na iwe hivyo, na kama ni ya malisho na iwe maalum kwa wafugaji na si vinginevyo.

Akiwasilisha dhumuni la Mkutano huo, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu (DLUPMC) Bw. Jonas Masingija Nestory kutoka Tume, ameeleza kuwa uwasilishaji wa Rasimu hiyo inalenga kupata maoni na mapendekezo ya wataalamu ambao yatasaidia kuleta tija na kuona namna vema ya kutumia ardhi ili kuongeza thamani ya rasilimali zinazotumia ardhi na kukuza uchumi kwa kuzingatia fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa.

Aidha, Mkurugenzi Masingija ameeleza kuwa, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na fursa za rasilimali ardhi zilizopo Mkoani hapo, katika kipindi cha miaka 20 ijayo,rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Mkoa umependekeza Shinyanga kuwa kitovu cha usindikaji wa mazao ya Mifugo, chakula na senta kubwa ya madini.

Uandaaji wa Mpango huo unatekelezwa chini ya Mradi wa Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kikanda, Mikoa, Wilaya na Vijiji (ZORED) unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea na Afrika (KOAFEC) kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).