Habari
Hatimiliki 1,022 zatolewa Ushetu

Wananchi zaidi ya 1,000 wa Vijiji vya Butibu na Igunda vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoani Shinyanga wamenufaika na Hati za Hakimiliki za Kimila mara baada ya kupimiwa vipande vyao vya ardhi na kumilikishwa kisheria kupitia Hati hizo hali itakayowahakikishia milki salama za ardhi, kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi pamoja na kuwainua kiuchumi pindi watakapozitumia kama dhamana.
Akiongea kwenye halfa ya kukabidhi Hati hizo iliyofanyika leo Septemba 25, 2025 katika Kijiji cha Igunda, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bw. Deus Kakulima Antony akimuawakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama ameishukuru Serikali kupitia Tume kwa kuwezesha wananchi wake kumiliki ardhi Kisheria.
Kwa upande wake, Mkurungenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu (DLUPMC) kutoka Tume, Bw. Jonas Masingija Nestory amesema kuwa uandaaji wa Hatimiliki hizo ni ukamilishaji wa zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya ardhi ya Vijiji katika hatua ya Tano na ya Sita inayotaka kuandaliwa kwa Mipango Kina (Detailed Land Use Plans) kwa ajili ya Usimamizi na Utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa katika hatua ya Kwanza hadi ya Nne.
Mkurugenzi Masingija alifafanua kuwa, hatua za awali za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi (1 – 4) ilihusisha kuwawezesha wananchi kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile Kilimo, Makazi, Malisho, Huduma za jamii na nyinginezo kulingana na mahitaji ya wananchi na uwezo wa rasilimali ardhi katika Vijiji husika, na sasa wamemalizia katika hatua za usimamizi wa maeneo hayo.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi hiyo Msimamizi wa Timu inayowezesha zoezi hilo kutoka Tume Bw. Otmary Komba ameeleza kuwa, Tume ilidhamiria kuwezesha uandaaji wa Hatimiliki 1,000 kwa Vijiji viwili vya Butibu na Igunda, lakini kwa juhudi na maarifa za Wataalamu wa Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, wamefanikiwa kuzidi lengo walilojiwekea.
Kufanyika kwa kazi hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project) unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) ambapo katika awamu hii, uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) pia unatekelezwa katika Vijiji viwili vya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.