Habari

Vijiji 48 kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Hatimiliki 2,000 kutolewa kwa Wananchi

Vijiji 48 kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Hatimiliki 2,000 kutolewa kwa Wananchi
Sep, 25 2025

Na. Moteswa Msita, Dodoma

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 7 inataraijia kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 48 huku Wananchi zaidi ya 2,000 wakitarajiwa kumilikishwa ardhi zao kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs).

Akizungumza Jijini Dodoma katika Kikao Kazi cha Wataalamu wa Tume watakaoshiriki katika utekelezaji wa kazi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph Mafuru, amewahimiza wataalamu hao kufanya kazi kwa nidhamu na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha matokeo ya kazi yao yanawanufaisha wananchi na kuchangia katika kujenga taswira chanya ya Taasisi pamoja na Serikali kwa ujumla.

“Ni muhimu kila mmoja wenu atambue wajibu wake katika zoezi hili. Nidhamu, uadilifu na uwajibikaji ni misingi muhimu katika utekelezaji wa kazi hii ili kuisaidia jamii kujiletea maendeleo na kwa upande wenu kutimiza wajibu wa Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi” alisisitiza Bw. Mafuru.

Awali, akitoa malengo ya kufanyika kwa kazi hiyo Mkurugenzi anayeshughulikia Uandaaji na Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi (DLUPMC), Bw. Jonas Masingija Nestory amesema kuwa, uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila unalenga katika Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na miradi ya Kimkakati.

Bw. Masingija aliendelea kueleza kuwa, Halmashauri za Wilaya nyingine zitakazo husika na zoezi hilo ni zile zilizopo mipakani na nchi jirani, pamoja na Vijiji vinavyokumbana na migogoro ya mara kwa mara, vikiwemo Vijiji 975 vilivyokuwa na migogoro na maeneo ya Hifadhi na kufanyiwa maamuzi na Baraza la Mawaziri.

Halmashauri zitakazonufaika na zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi kwa awamu hii ni Nanyumbu, Mtama, Bahi, Sikonge na Nyang'hwale. Aidha, wananchi zaidi ya 2,000 waliopo kwenye Vijiji vinne (4) vya Halmashauri za Wilaya za Rungwe na Ushetu, watanufaika na umilikishwaji wa maeneo yao kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila.

Zoezi hilo linalotarajiwa kuanza Septemba 15, 2025, linafanyika kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume kupitia fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.