Habari

Vijiji 23 Vyanufaika na Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kupitia Mradi wa FORVAC

Vijiji 23 Vyanufaika na Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kupitia Mradi wa FORVAC
Nov, 09 2019

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Mradi wa Kuongeza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) pamoja na Halmashauri za Wilaya imekamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 23 vilivyopo katika Wilaya tisa (9) zinazounda Kongani (Clusters) tatu za Tanga, Ruvuma na Lindi.

Mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Divisheni ya Misitu na Nyuki, unategemewa kutekelezwa kwa muda wa miaka minne (2018 – 2022) na unalenga kuongeza mnyororo wa thamani kupitia mazao yanayotokana na misitu ili kuboresha maisha ya wananchi waliopo kwenye vijiji vyenye hifadhi za misitu ya vijiji nchini.

Akizungumza katika kikao kazi cha uwasilishaji wa kazi zilizofanyika uwandani pamoja na kuhakiki taarifa za kazi hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Dkt. Stephen Nindi amewataka wataalamu kuhakikisha wanazitendea haki kazi za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ngazi ya vijiji kwa kuzingatia Sheria na miongozo ya upangaji, utekelezaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi, kwani ubora wake ndio kielelezo cha utaalamu wao ambao matokeo yake yatapelekea kubadilisha maisha ya wananchi wa vijijini kiuchumi.

“Nyinyi kama wataalamu, lazima mpitie vizuri mipango hii ili kuepuka kuwepo na makosa ambayo yalijitokeza wakati wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kule vijijini hatua ambayo itafanya kusiwepo wa kuhoji ubora wake huko mbele wakati mipango hii inawasilishwa kwenye hatua nyingine za kuitangaza kwenye gazeti la Serikali” Alisema Dkt. Nindi.

Kwa upande wake, Meneja wa programu ya FORVAC anayeshughulikia misitu na mnyororo wa thamani Bwana Alex Njahani, amedokeza kuwa miaka mawili ya mwanzo ya programu hiyo itakuwa ni ya upangaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi ngazi ya vijiji itakayolenga kufikia takribani vijiji 57 kwa lengo la kupata matokeo yanayokusudiwa.

“Mradi huu ni wa miaka minne (4) lakini, katika miaka miwili (2) ya mwanzo shughuli zitakazofanyika zitalenga katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyokusudiwa 57, ambapo tunataka kuhakikisha mipango hiyo inafikia hatua ya uandaaji wa mipango kina kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za misitu za vijiji kwa lengo la kuboresha shughuli za wananchi kwenye maeneo haya ili kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na misitu” alieleza Bw. Njahani.

Sambamba na hilo, Bwana Njahani alisisitiza umuhimu wa kuhakiki kazi hizo ili ziende kwenye hatua zinazofuata za kupitishwa kwenye Baraza la Madiwani katika kila Wilaya husika na baadae mipango hiyo kusajiliwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali ili kuendelea na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyosalia.

Wilaya na vijiji vilivyonufaika na awamu ya kwanza ya mradi huo ni pamoja na Nyasa (Hinga, Litumbakuhamba na Litoromelo), Mbinga (Kindimba juu, Kindimba chini na Ndongosi), Songea (Kikunja, Liweta na Litowo) na Namtumbo (Limamu na Kumbara) katika Mkoa wa Ruvuma. Wilaya na vijiji vingine ni Ruangwa (Chingumbwa, Machang’anja na Mmawa), Liwale (Turuki na Likombora) katika Mkoa wa Lindi, pamoja na Handeni (Kwamsundi na Kitumbi), Kilindi (Tuliani Kwedijero, Komnazi na Mkonde), Mpwapwa (Chiseyu na Ikuyu) katika Mkoa wa Dodoma.

Zoezi hilo linategemea kuendelea kwenye Wilaya hizo mara baada ya uchaguzi wa viongozi wa Serikali za vijiji (Serikali za Mitaa) kukamilika, kwani hatua za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni shirikishi, na huanzia katika ngazi ya uongozi wa Halmashauri katika vijiji husika