Habari
Baraza la Wafanyakazi NLUPC Lapitisha Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2025/2026

Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) limepitia, kujadili na kupitisha Mpango wa Bajeti wa Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026 huku wajumbe wakihimizwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya Taasisi.
Mpango huo wa Bajeti wa Tume ulioangazia kazi mbalimbali zinazotarajiwa kutekelezwa na Tume kwa mwaka ujao wa fedha, umepitishwa Februari 28, 2025 wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza hilo Bw. Joseph Mafuru, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Tume, amewahimiza wajumbe hao kurudisha mrejesho kwa watumishi wanaowawakilisha na kuwataka kufanya kazi kwa bidii kutekeleza mpango huo, pamoja na kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kutimiza malengo ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Vilevile, Menejimenti ya Tume imeahidi kuifanyia maboresho Bajeti hiyo kupitia maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na wajumbe wa Baraza hilo ili kutekeleza dhana ya uandaaji wa Bajeti Shirikishi, ambayo husaidia katika kurahisisha utendaji kazi wa Taasisi.
Bajeti hiyo inategemewa kutumika katika matumizi ya kawaida ya Tume kwa ajili ya Mishahara, Matumizi mengineyo pamoja na Miradi ya Maendeleo kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Planning Project).