Habari
Bilioni 5 kutekeleza Proramu ya Kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Na Eleuteri Mangi
Bunge limeazimia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kupewa kiasi cha Sh. 5,000,000,000 ili kutekeleza Programu ya Kuandaa Mipango wa Matumizi ya Ardhi kwa Vjijiji 333.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii kukutana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Fedha Februari 04, 2025 ambapo Wizara ya Ardhi ilitekeleza kwa ufanisi programu ya kuandaa matumizi ya ardhi kama ilivyokusudiwa na kuifanya sekta ya ardhi kuendelea kuleta ustawi wa wananchi.
Akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati kwa kipindi cha Februari, 2024 hadi Januari, 2025 Bungeni jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema, kamati yake imewasilisha taarifa hiyo baada ya kutembelea na kukagua miradi na utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
"Katika kutekeleza Proramu ya Kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi kwa Vjijiji 333 kwa mwaka wa Fedha 2024/2025, Wizara ya Ardhi ilipanga kutekeleza programu maalumu ya kupanga vijiji 333 ambapo kiasi cha Shilingi 5,000,000,000 kilipangwa kutekeleza program hiyo. Amesema
Akichangia taarifa hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Wizara yake itatekeleza maazimio yote yaliyotolewa na Bunge sambamba na kuhakikisha mifumo yote inasomana.
“Maazimio ya Bunge ni sauti za wananchi ambao wananshauri nini kifanyike katika sekta hii, sisi tunaenda kuhakikisha mifumo inasomana, tunaenda kuhakikisha halmashauri zote 184 zinapata mfumo wa e-Ardhi” amesema Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake Mhe. Dkt. Florence Samizi amesema upo umuhimu wa kupanga matumizi bora ya ardhi nchini na kuiomba Serikali iendelee kupeleka fedha katika Tume ya Kitaifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ili iweze kupanga vijiji vyote nchini.