Habari
KM Sanga aipongeza Tume kwa Upangaji na Usimamizi wa Ardhi Nchini
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameipongeza Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kutokana na kazi kubwa inayofanya ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina imani kubwa na kazi za Tume kutokana na kuisaidia wizara na hasa katika maeneo ya migogoro ya vijijni ikiwemo ya wakulima na wafugaji.
"Nikiri kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua sana tofauti na ilivyokuwa miaka ya zamani maana tulikuwa na kesi nyingi za hii migogoro lakini kwa kiasi kikubwa imepungua”. Amesema.
Mhandisi Sanga ametoa pongezi hizo tarehe 17 Desemba 2025 wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Akizungumzia kuhusu Kamati ya Ufundi ya Matumizi ya Ardhi, Mhandisi Sanga amesema sekta mtambuka kupitia Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi anaamini sasa migogoro ya ardhi inaenda kupungua.
Aidha, ameipongeza Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Kamati ya Ufundi kwa ajili kutoa ushauri kuhusu Upangaji na Usimamizi wa Matumizi ya ardhi nchini.
Amesema, uamuzi wa kuwa na chombo hicho cha ufundi ni hatua ya msingi katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na mifumo thabiti, madhubuti na endelevu ya matumizi ya ardhi yanayochangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutawala.
Kamati ya Ufundi ya Matumizi ya Ardhi imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura ya 116, kifungu cha 19 na kifungu kidogo cha 5 ikiwa na lengo la kushauri masuala ya kiufundi ya utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.
