Habari

Waziri Mkuu Ataka Uwekezaji zaidi katika Mipango ya Matumizi ya Ardhi kukomesha Migogoro

Waziri Mkuu Ataka Uwekezaji zaidi katika Mipango ya Matumizi ya Ardhi kukomesha Migogoro
Mar, 03 2026

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuwekeza kwa nguvu katika uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi akisema kuwa hiyo ndiyo njia ya kudumu ya kuondokana na migogoro ya mara kwa mara ya ardhi inayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana Jumatatu, Machi 2, 2026, wakati akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara yake mkoani Manyara Region kilichofanyika Wilayani Mbulu.

Amesema kuwa changamoto ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na watumiaji wengine wa ardhi haitapatiwa suluhisho la kudumu bila kuwepo kwa mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi inayotekelezwa na kusimamiwa ipasavyo.

“Ardhi haiongezeki, bali binadamu ndiyo wanaongezeka. Hivyo, ni lazima tupange matumizi yake kwa busara ili kila mmoja apate nafasi ya kufanya shughuli zake bila kuingiliana,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utoaji wa elimu kwa wananchi ili watambue na kuzingatia matumizi yaliyopangwa katika maeneo yao. Alieleza kuwa mipango ya matumizi ya ardhi haina maana endapo jamii haitapatiwa uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wake na wajibu wao katika kuitekeleza.

Pia alitoa rai ya kuheshimu shughuli za kila kundi, hususan wakulima na wafugaji, akisema kuwa sekta zote ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na zinapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia mipaka na makubaliano yaliyowekwa.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kutumia busara, mila na uungwana katika kutatua migogoro ya ardhi badala ya kuchukua sheria mkononi, huku akiwataka viongozi wa ngazi zote kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuleta amani na maendeleo endelevu.

Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Manyara imelenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.