Habari
Mpunga kuongezewa thamani kupitia Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Uhifadhi wa Mazingira
Katika kuhakikisha zao la mpunga linazalishwa kwa wingi na kuongezewa thamani, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia mradi wa Food Systems, Land Use and Restoration (FOLUR), imeanza kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji inayolenga kuimarisha usimamizi jumuishi wa rasilimali za ardhi, maji na mazingira katika Kongani ya Kilombero, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.
Mradi huo unaotekelezwa katika vijiji 23 vya Mlimba pamoja na Wilaya za Kaskazini A na B, Zanzibar, unalenga kuunganisha uzalishaji wa kilimo, uhifadhi wa mazingira na upangaji wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya maendeleo endelevu. Kupitia utekelezaji wake, zoezi la utambulisho wa uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi limefanyika katika vijiji vya Luvilikila, Isago na Mkangawalo, hatua inayowezesha kutengwa kwa maeneo ya matumizi mbalimbali ya ardhi ikiwemo kilimo, makazi, malisho na maeneo ya hifadhi.
Sambamba na hilo, zoezi la kuandaa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) 500 kwa wananchi wa Kijiji cha Luvilikila linaendelea. Zoezi hilo linalenga kuhakiki na kupima vipande vya ardhi vya wananchi ili kuwamilikisha rasmi, hatua itakayochangia kuimarisha usalama wa miliki za ardhi, kuongeza uwekezaji katika kilimo cha mpunga na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi.
Akizungumza wakati wa kuanza kwa zoezi hilo, Msimamizi wa shughuli hiyo na Mkuu wa Kanda ya Mashariki kutoka NLUPC, Bw. Edward Mpanda, alisema mradi huo unalenga kuongeza thamani ya zao la mpunga kupitia usimamizi bora wa ardhi, matumizi ya mbinu za kilimo rafiki kwa mazingira pamoja na urejeshwaji wa maeneo yaliyoharibika ili kulinda vyanzo vya maji na bioanuwai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Luvilikila, Bw. Bukula Joseph, alisema utekelezaji wa mpango huo utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi na wakati huo huo kuimarisha utunzaji wa mazingira na maeneo oevu, ambayo ni muhimu kwa uzalishaji endelevu wa zao la mpunga.
Wananchi wa Luvilikila wameeleza kuwa kupitia uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, kutengwa kwa maeneo ya uhifadhi pamoja na utoaji wa Hatimiliki za Kimila, Kijiji kitapata uwiano mzuri kati ya uzalishaji wa kilimo na ulinzi wa mazingira.
Kupitia ushirikiano huo, NLUPC na Wizara ya Maliasili na Utalii wanalenga kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kwa njia endelevu, kulinda misitu na vyanzo vya maji, pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi ya ardhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
