Habari
Waziri Akwilapo aagiza kuongezwa kasi ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Nchini
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameiagiza Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kuongeza kasi ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kilimo, makazi na uwekezaji.
Mhe. Dkt. Akwilapo ametoa agizo hilo tarehe 17 Desemba 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (Land Use Planning Technical Committee) kilichofanyika katika Makao Makuu ya Wizara Jijini Dodoma.
Kupitia kikao hicho, Waziri amehimiza matumizi makubwa ya teknolojia katika ukusanyaji wa takwimu za upangaji ardhi, ulinzi wa maeneo nyeti ya ikolojia yakiwemo misitu, vyanzo vya maji na njia za wanyamapori, pamoja na kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kupitia mipango shirikishi na endelevu.
Amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali za matumizi ya ardhi, ikiwemo migongano kati ya shughuli za kilimo na ufugaji, migongano kati ya malisho na uhifadhi, pamoja na upungufu wa maeneo ya uwekezaji wa kimkakati unaosababishwa na mabadiliko ya matumizi ya ardhi yasiyopangwa.
Changamoto nyingine alizozitaja ni uharibifu wa mazingira unaotokana na uvamizi wa vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo, matumizi yasiyo rasmi ya ardhi, athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuongeza shinikizo kwa ardhi na rasilimali zake, pamoja na ukuaji wa haraka wa miji unaohitaji mipango bunifu na matumizi bora ya ardhi.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Mhe. Dkt. Akwilapo amesema Serikali inategemea utaalamu na ushauri wa Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ili kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija, usawa, usalama na uendelevu.
“Ninaamini ushauri wa Kamati utakuwa mhimili muhimu wa kuimarisha sera, miongozo na taratibu zinazohusu matumizi ya ardhi nchini,” amesema Mhe. Dkt. Akwilapo, akiongeza kuwa ameielekeza Tume kuwa makini katika kusaidia Kamati kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuepusha migongano katika utekelezaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amesema Wizara ina imani kubwa na kazi zinazofanywa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, hasa katika kusaidia utatuzi wa migogoro ya ardhi Vijijini, ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Ni dhahiri kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo kulikuwa na idadi kubwa ya kesi zinazohusiana na migogoro hiyo,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Bw. Joseph Mafuru, amesema Tume itahakikisha Kamati ya Ufundi inatekeleza majukumu yake kwa weledi, huku akieleza imani yake kuwa wajumbe walioteuliwa wataziwakilisha vyema Taasisi walizotoka kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Ameeleza kuwa katika kipindi ambacho Tume ilikuwa bila Kamati, ilikosa fursa muhimu ikiwemo kupata ushauri wa kitaalamu unaoratibiwa kimfumo katika sekta mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi kama vile kilimo, mifugo, misitu, utalii, ujenzi, uwekezaji na tafiti.
Kwa mujibu wa Bw. Mafuru, changamoto nyingine zilizojitokeza ni kukosekana kwa mkakati wa pamoja wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, upungufu wa takwimu za pamoja, mapungufu katika uratibu wa Taasisi, pamoja na ukosefu wa viwango vya Kitaifa vya mipango ya matumizi ya ardhi.
Kamati hiyo ya Ufundi inaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 19(5) cha Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Sura 116 ikiwa na jukumu la kuishauri Tume kuhusu masuala ya kisekta yanayohusu Uandaaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya ardhi nchini.
