Habari
Fahamu kuhusu Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995, Toleo la Mwaka 2023

Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 Toleo la Mwaka 2023 ilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Machi 17, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Katika uzinduzi huo, Tume ilikuwa ni miongoni mwa Taasisi zilizoshiriki kikamilifu kwenye hafla hiyo pamoja na maonesho yaliyofanyika kwenye viunga vya ukumbi huo. Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi, Sura 116, Tume ndio Mratibu wa Uandaaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.
Pamoja na masuala mengine yaliyomo kwenye Sera hiyo, masuala ya Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi yamezingumziwa katika muktadha mbalimbali.
Kwanza, katika kuangalia utekelezaji wa Sera hiyo toka ilipoanza kutumika mwaka 1995, Sera hiyo imetambua kazi kubwa iliyofanyika katika uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji.
Kwa mujibu wa aya 1.2.4.2 ya Sera hiyo, imetambua utungwaji wa Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi, Sura 116 ili pamoja na mambo mengine kuhamasisha ushiriki wa umma na sekta binafsi katika shughuli zinazohusiana na upangaji wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya matumizi ya ardhi yenye uwiano na manufaa kwa wadau wote.
Aidha, Miongozo iliandaliwa na kusambazwa ili kuwawezesha wadau katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Vijiji kushiriki kikamilifu katika utayarishaji na utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
Vilevile, Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (2013-2033) uliandaliwa ambao unatoa Mwongozo wa utayarishaji wa Mipango ya Matumizi ya ardhi katika ngazi za Mikoa na Wilaya. Mpango huu una Programu 12 za utekelezaji na unaendelea kutekelezwa kwa awamu na sekta zote katika maeneo mbalimbali nchini.
Sera imekiri kuwa kutokana na jitihada hizo, zimewezesha kuandaliwa kwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji 2,944 kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini. Uwepo wa mipango hii umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya matumizi na mipaka ya vijiji.
Vilevile, haki za kumiliki ardhi zinatambulika na kuheshimiwa wakati wa kutoa haki kwa watumiaji wa rasilimali za asili kwa utaratibu wa matumizi shirikishi. Kadhalika, mipango ya matumizi ya ardhi huzingatia utengaji wa maeneo kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, umeme na maji
Pili, Sera ya Taifa ya Ardhi Toleo la Mwaka 2023 imeweka lengo lenye Matamko mawili kuhusu uandaaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi nchini. Kwa mujibu wa aya ya 3.6.1, Sera imeweka lengo Kuimarisha Mfumo wa uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi Vijijini.
Sera imeweka lengo kwamba Serikali itahakikisha kuwa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji inaandaliwa na kutekelezwa pamoja na kuweka utaratibu utakaowezesha wadau kushiriki katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi zote.
Sera imeweka lengo na matamko hayo ili kuhakikisha kunakuwepo na kasi ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi, kupunguza athari za mazingira na migogoro ya matumizi ya ardhi pamoja na kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapangiwa matumizi, kupimwa na kumilikishwa kwa mujibu wa Sheria.