Habari
Hati 1,000 Kutolewa kwa Wananchi pembezoni mwa Misitu ya Hifadhi

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeanza kazi ya kuwezesha uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) zaidi ya 1,000 kwa wananchi wa Vijiji 4 vinavyopakana na Hifadhi za Misitu ya jamii ya Miombo vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya ya Sikonge, Urambo na Kaliua Mkoani Tabora.
Kazi hii inafanyika ikiwa ni muendelezo wa juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya uhifadhi nchini, mara baada ya Vijiji 14 vinavyopakana na safu za Misitu ya Miombo iliyopo ukanda wa Tabora (Kaliua landscape) na Katavi (Mlele Landscape) kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyopelekea Hatimiliki 223 kutolewa kwa wananchi wa Kijiji cha Mtakuja kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mkoani Katavi.
Lengo kuu la utoaji wa Hatimiliki hizo kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za misitu ni kuimarisha Usalama wa Milki za Ardhi na kupunguza migogoro baina ya jamii na mamlaka za hifadhi na kufanya uhifadhi endelevu kwa njia shirikishi.
Pia, zoezi hili linatarajiwa kuchangia katika kulinda na kuhifadhi misitu na rasilimali asilia kwani Wananchi wakitambuliwa kisheria kuwa wamiliki wa ardhi iliyo jirani na hifadhi, watakuwa na hamasa kubwa ya kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kulinda mazingira.
Vilevile, umiliki rasmi wa ardhi unawapa wajibu wa kutambua mipaka ya maeneo yao na kuhakikisha kuwa shughuli za kibinadamu hazileti athari mbaya kwa mifumo ya ikolojia, na hivyo kusaidia juhudi za Taifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande mwingine, Wananchi wanatarajiwa kutumia Hatimiliki hizo kupata mikopo kwenye Taasisi za fedha na kutumia mikopo hiyo kukuza uwekezaji na kuboresha uzalishaji katika shughuli endelevu za kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo zinazotokana na mazao ya misitu.
Kazi hii inafanyika kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame Tanzania (Integrated Landscape Management in Dry Miombo Woodlands of Tanzania) unaotekelezwa za TFS kwa Ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Kimataifa (GEF) na Shirika la Chakula Duniani (FAO).