Habari
Hatimiliki 369 zaandaliwa Kilolo

Jumla ya Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) 369 zimeandaliwa kwenye Kijiji cha Vitono kilichopo Kata ya Uhambingeto, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mara baada ya Kijiji hicho kuwezeshwa kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi na baadae kuandaliwa Mpango Kina (Detail Land Use Plan) uliopelekea kupima maeneo na kuandaa Hatimiliki hizo.
Zaidi ya Wananchi 185 walijitokeza na kukabidhiwa Hatimiliki hizo na Katibu Tawala Wilaya ya Kilolo Ndg Estomin Kyando kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye hafla fupi iliyofanyika Kijijini Vitono.
Hatimiliki hizo zimeandaliwa kupitia Mfumo wa kielektroniki unaotumika kuhifadhi Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUIS) ambapo pamoja na mambo mengine, baada ya kuwepo kwa mpango wa matumizi ya ardhi ya Kijiji unawezesha kupima maeneo na kuandaa Hati za Hakimiliki za Kimila.
Baadhi ya wananchi waliokabidhiwa Hatimiliki hizo wameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyowezesha zoezi hilo na kueleza kuwa Hatimiliki hizo zitawasaidia kuwa na milki salama za ardhi zao na wanakusudia kuzitumia vizuri ili kujikwamua kiuchumi.
Aidha, wananchi hao wamegusia juu ya umuhimu wa Hatimiliki hizo katika kuthibiti ongezekao la migogoro ya ardhi kwa kuwa kila mtu atajua mwanzo na mwisho wa eneo lake hali itakayosaidia kupunguza migogoro isyokuwa ya lazima.
Katika awamu hii, kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project) Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo imewezeshwa kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 10 vikiwemo Vijiji vinavyopitiwa na Vyanzo vya maji vinavyosaidia ujazaji maji kwenye bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP).