Habari
Hatimiliki 580 zamilikisha Ardhi Sikonge kupitia Mradi wa DSL - IP
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imewezesha uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) 580 kwa Wananchi wa Vijiji vya Makibo na Zugimlole vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo (DSL-IP) unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Shirika la Chakula Duniani (FAO) na kuratibiwa na TFS, ili kuimarisha usalama wa milki za ardhi na kupunguza migogoro kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa ugawaji wa Hati hizo kwa Wananchi uliofanyika Oktoba 25, 2025 katika Kijiji cha Makibo, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Thomas Myinga, alisema kuwa Hati hizo zitawawezesha wananchi kuwekeza katika shughuli endelevu za uzalishaji mali, kama vile kilimo, ufugaji na biashara hatua itakayochochea kukua kwa uchumi wa kaya na kulinda mazingira.
“Mipango hii na Hati hizi ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza upotevu wa bioanuwai na uharibifu wa ardhi. Tunataka kuona jamii zikiwekeza katika matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa misitu ya miombo,” alisema Myinga.
Mkuu huyo wa Wilaya, aliwasisitiza wananchi kuheshimu na kuyatumia vizuri maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ili kuepuka migogoro baina ya makundi mbalimbali ya watumiaji ardhi pamoja na mamlaka zinazosimamia hifadhi ili kuleta tija na dhamana ya mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa.
Aidha, Mhe. Myinga alieleza uhusiano wa utekelezaji wa kazi hiyo na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa hivi karibu na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo pia imezungumzia masuala ya Uhifadhi, Mabadiliko ya Tabia nchi, Upangaji Matumizi ya Ardhi pamoja na Umilikishaji wananchi kupitia Hatimiliki.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Dkt. Zainab Bungwa, alisema mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 6.8 (sawa na Sh bilioni 16.8) unatekelezwa kwa miaka mitano (2023–2027) katika Wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge (Tabora) na Mlele (Katavi) kwa lengo la kurejesha uoto wa asili, kupunguza uharibifu wa ardhi na kuboresha maisha ya wananchi.
Dkt. Bungwa alisema kuwa pamoja uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi kupitia mradi huo, TFS pia inatekeleza kazi mbalimbali zikiwemo ujenzi wa vituo vya ulinzi wa misitu (Ranger Posts), matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) kwa ulinzi, ujenzi wa nyumba za nyuki, maghala ya mbegu na miundombinu ya maji kwa ajili ya jamii zinazoshiriki uhifadhi.
Awali, akitoa taarifa juu ya utekelezaji wa kazi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume Bw. Joseph C. Mafuru, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Mipango ya Matumizi ya Ardhi kutoka Tume Bw. Obed Katonge alisema kuwa Tume itaendelea kushirikiana na Mamlaka za upangaji ili kuhakikisha ardhi inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa wananchi, huku akisisitiza wananchi kulinda Hati zao na kuepuka kuazimishana, kwani kufanya hivyo ni kuvunja Sheria.
Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa, katika uetekelezaji wa Mradi huo, Tume kwa kushirikiana na TFS pamoja na Mamlaka za Upangaji, imetekeleza kazi mbalimbali zikiwemo za Utatuzi wa Migogoro ya Mipaka kati ya Vijiji na Vijiji; kati ya Maeneo ya Wananchi na Maeneo ya Hifadhi, Uandaaji wa vyeti vya Ardhi vya Vijiji pamoja na kuwezesha wananchi kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali kulingana na mahitaji yao.
Aidha, katika zoezi la uandaaji wa Hati, takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya Hati za Hakimiliki za Kimila 580 zimeandaliwa katika Vijiji viwili vya Makibo (339) na Zugimlole (241) ambazo zimezingatia makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo Wanaume 427 (73.62%), Wanawake 124 (21.38%), Umiliki wa pamoja 29 (5%) na wenye ulemavu 6 (1.03%).
“Hati hizi zitaimarisha Usalama wa Milki za Ardhi na kupunguza migogoro baina ya jamii na mamlaka za hifadhi na kufanya uhifadhi endelevu kwa njia shirikishi na hivyo, kukuza uwekezaji katika shughuli endelevu za kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo zinazotokana na mazao ya misitu.” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu
Kuvuka lengo la uandaaji wa Hati hizo ni mojawapo ya mafanikio yaliyoainishwa kwenye taarifa hiyo ya Mkurugenzi Mkuu ambapo, hapo awali, lengo lilikuwa ni kuandaa Hatimiliki za Kimila 300, lakini kwa mchango wa rasilimali fedha na rasilimali watu kutoka Tume, Hatimiliki zingine 280 ziliandaliwa iliyopekea kuvuka lengo na kufikia Hati 580.
Vilevile, alidokeza kuwa kazi hiyo imefanyika kwa ufanisi na kasi kutokana na matumizi ya Mfumo wa Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUIS) unaowezesha kukusanya taarifa mbalimbali za wamiliki, kupima maeneo pamoja na kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila hali inayosaidia zoezi hilo kufanyika kwa haraka huku likifuata taratibu zote zilizoainishwa Kisheria.
Kufanyika kwa kazi hiyo ni juhudi za Serikali kuendeleza na kulinda Sekta ya Uhifadhi, kupunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi kupitia usimamizi shirikishi wa safu za misitu ya miombo iliyopo kwenye ukanda wa Kaliua na Mlele.
