Habari
Kamati ya Bunge yataka Rombo kupewa kipaumbele Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Na Joel Magese, Rombo, Kilimanjaro
Kamati ya Kudumu ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava imeitaka serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuipa kipaumbele Halmashauri ya Wilaya ya Rombo katika uandaaji wa Mipango wa Matumizi bora ya Ardhi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe, Timotheo Mzava tarehe 15 Machi 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kisale Msalanga katika ziara ya kamati iliyokwenda kukagua mradi wa upangaji wa matumizi ya Ardhi katika halmashauri ya Wilaya ya Rombo iliyopo Mkoani Kilimanjaro.
Kadhalika Mhe. Mzava amekabidhi Jumla ya hakimiliki za kimila 390 kwa wananchi hao ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ibara ya 74 inayoelekeza kuandaa mipango ya matumizi ya Ardhi, Kuandaa mipango kina katika kuimarisha salama za miliki kwa kuwezesha utoaji wa hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amesema, zoezi la upangaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji 24 kati ya 68 vya halmashauri ya wilaya ya Rombo ni suluhisho la migogoro ya Ardhi na mipaka katika vijiji hivyo kwani tayari vimekwisha wekewa mpango wa matumizi bora ya Ardhi.
Vilevile mhe. Pinda amekemea vikali vitendo vya baadhi ya wenyeviti wa vijiji wasio waadilifu kwa kujishughulisha na uuzaji wa maeneo ya vijiji kiholela na hivyo kuchochea migogoro ya Ardhi.
Katika Mwaka wa fedha 2024/25 Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliidhinishiwa jumla ya Tsh. bilioni 5 ili kuweza kutekeleza kazi za Maendeleo kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi (Land Use Planning Project) kwenye Vijiji 280 katika maeneo yaliyopitiwa na Miradi ya Kimkakati ya Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) na Reli ya Kisasa (SGR), maeneo yenye migogoro katika vijiji 975 vyenye maelekezo ya Baraza la Mawaziri pamoja na Vijiji vilivyopo mipakani mwa nchi.