Habari
Karibuni mtuondolee kero za Migogoro ya Ardhi – DC Ukerewe

Na Moteswa Msita, Ukerewe, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Christopher Ngubiagai ameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa wataalamu wake kufika Wilayani humo kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji, hatua itakayowezesha kutatua kero za migogoro ya matumizi ya ardhi iliyokithiri katika Wilaya yake.
Akizungumza na wataalamu hao Ofisini kwake, Mhe. Ngubiagai ameeleza kuwa katika kipindi chake cha kuhudumu kwenye Wilaya hiyo, ameshuhudia mlundikano wa kesi Mahakamani zinazohusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi ambapo kwa ujuo wa zoezi hilo utakuwa ni mwarobaini utakaowezesha wananchi wake kuendelea na shughuli za maendeleo badala ya kushinda Mahakamani.
“Ukija kwenye Mahakama zetu migogoro ya ardhi ndio inayoongoza katika mashauri ambayo yamerekodiwa hapa Wilayani, kwa hiyo ujio wa Tume na uamuzi uliofanyika wa kuiweka Ukerewe kwenye zoezi la uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji ni jambo jema kwani litaenda kutatua kero za migogoro ya ardhi katika Vijiji vya Halmashauri yetu ya Ukerewe” alisisitiza Mhe. Ngubiagai.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Bw. Goodluck Mtigandi ametambua umuhimu na upekee wa zoezi hilo na kuahidi kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika ili kufanikisha kazi hiyo katika Halmashauri bila kikwazo chochote.
Awali, akitoa taarifa ya utaratibu wa utekelezaji wa kazi hiyo kwa Viongozi hao wa Wilaya, Mkuu wa Kanda ya Ziwa kutoka Tume, ambaye pia ni Kiongozi wa Timu Bw. Abdallah Magombana, amesema kuwa, katika Wilaya hiyo, zoezi hilo litajumuisha jumla ya Vijiji 16 kwa awamu 2, kila awamu itakuwa na Vijiji 8.
“Zoezi hili litafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itajumuisha Vijiji 8 vya Namagondo, Busunda, Igongo, Muhande, Busiri, Bwasa, Mukasika na Kijiji cha Chankamba” alieleza Bw. Magombana na kuendelea kuwa awamu ya pili itajumuisha Vijiji vya Mibungo, Kigala, Busagami, Kaseni, Buzwege, Buguza, Chamuhunda pamoja na kijiji cha Mahande”.
Zoezi hilo litakalofanyika kwa takribani siku 30 katika Wilaya hiyo, litahusisha utoaji elimu kwa wananchi juu ya usimamizi wa Rasilimali Ardhi, Utengaji wa maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kadri ya mahitaji ya wananchi pamoja na uhuhishaji wa mipaka ya Vijiji pale itakapohitajika.
Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina jumla ya Vijiji 76, ambapo kwa mara ya kwanza Vijiji 16 kati ya hivyo vinawezeshwa kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Aidha, Wilaya hiyo ni moja kati ya Wilaya zilizopo mipakani mwa Tanzania na nchi jirani, hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa Wilaya 21 ambazo Vijiji vyake vinaandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji.