Habari
MAFURU: Zingatieni Ushauri wa Wataalamu wa Afya

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Bw. Joseph Mafuru amewataka watumishi wa Tume hiyo kuzingatia ushauri wa Wataalamu wa Afya ili kuwa na mwenendo mzuri wa mtindo wa maisha hali itakayosaidia kuleta tija mahali pa kazi.
Bw. Mafuru ameyasema hayo Machi 28, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa Tume kuhusu Magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiambukiza, Afya ya Akili pamoja na Lishe yaliyofanyika ofisi za Makao Makuu ya Tume, Jijini Dodoma.
“Watumishi kuwa na afya njema ni mtaji mkubwa sana katika utendaji kazi, maana ndio msingi wa kutoa kazi bora. Changamoto za afya zina matokeo mabaya kwa Taifa na familia, hivyo ni vyema kusikiliza vizuri ushauri wa wataalamu wetu wa afya na kutekeleza ushauri huo” alisisitiza Bw. Mafuru.
Mkurugenzi Mafuru pia aliahidi kuendelea kuwezesha mafunzo kama hayo kila mara kwa kuwa pamoja na masuala mengine, mafunzo hayo husaidia watumishi kuboresha utendaji kazi kutokana na fikra chanya zinazojengeka kupitia mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Madaktari na wataalamu wa Lishe na Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma (DRRH), pamoja na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMH) yamefanyika ikiwa ni jitihada za Tume kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na mazingira bora ya kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.